Wednesday, January 08, 2014

Zitto aibuka kidedea mahakamani



Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto na wale wa uongozi wa juu, jana walipambana tena mahakamani kwa ngumi na mawe kisha kusababisha watu wawili kujeruhiwa.PICHA|MAKTABA 

Zitto Kabwe akipeana mikono na Wakili wa CHADEMA,Tundu Lisu baada ya kukibwaga chake chake.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda maombi yake dhidi ya chama hicho mahakamani.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando alikuwa akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana na maombi na hoja za Zitto na kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili na kutoa uamuzi wowote kuhusiana na uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa mgogoro baina ya pande mbili, hasara au madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa katika athari kwa pande zote.
Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa iwapo Mahakama haitaingilia kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.
Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja ya mtoa maombi kuathirika pamoja na wananchi wa jimbo lake kwa kukosa uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza ubunge kwa kuvuliwa uanachama utaitishwa uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema uchaguzi mdogo huwa unachukua mchakato mrefu.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi kuhusiana na uanachama wake kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya msingi,” alisema Jaji Utamwa.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya Chadema iliyotolewa na Wakili Kibatala baada ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando ambaye alidai kuwa katika hati hiyo, kuna taarifa za kusikia ambazo hakueleza alipozitoa.
Huku akirejea vifungu vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa Mahakama mbalimbali, alisisitiza kuwa ingawa wakili anaweza kuapa kwa niaba ya mteja wake, lakini anapaswa kueleza chanzo cha taarifa anazozitoa katika kiapo hicho.
Baada ya kutupilia mbali kiapo hicho, Jaji Utamwa alisema hata vielelezo vya wajibu maombi vinakufa kifo cha kawaida na kwa hali hiyo, maombi ya mtoa maombi yanabaki bila kupingwa na kwamba hakuna haja pia ya kujadili hoja za upande wa wajibu maombi.
Baada ya Jaji kutoa uamuzi huo, Zitto, aliwafuata mawakili wa Chadema na kupeana nao mikono kisha akaongozwa na walinzi wake kutoka nje ya Ukumbi wa Mahakama akipitia mlango maalumu unaotumiwa na jaji.
Kabla ya hukumu
Zitto aliyekuwa amevalia suti ya kijivu na shati la michirizi myeupe na ya kijivu aliwasili mahakamani hapo saa 7:45 mchana akiongozana na walinzi wake binafsi (mabaunsa), wapambe na wakili wake.
Baada ya kufika alikwenda katika chumba maalumu ambako alipumzika hadi saa 9:45 alasiri alipoingia katika ukumbi na kukaa katikati ya wapambe wake huku nyuma yake wakiwapo walinzi wake.
Jaji Utamwa aliingia mahakamani saa 9:56 alasiri na kuanza kusoma uamuzi wake akianzia na pingamizi la Zitto kwenye hati ya kiapo kinzani cha Chadema kisha akamalizia na uamuzi wa maombi ya msingi. Hukumu hiyo ilimalizika kusomwa saa 11:10 jioni.
Baada ya hukumu
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Msando alisema wameupokea kwa furaha uamuzi huo wa mahakama na kwamba hiyo ni hatua mojawapo ya haki akisema anaamini kuwa mteja wake atapata haki anayoitafuta.
Hata hivyo, Lissu na Kibatala kwa nyakati tofauti walisema kuwa ingawa wanakubaliana na uamuzi huo, hajawaridhika. SOURCE: MWANANCHI.

No comments: