WIZARA ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kesho itaanza kuwagawa samaki aina ya jodari waliokamatwa kwenye meli ya uvuvi ya MV Tawariq 1 wakivuliwa kiharamu.
Taasisi zitakazopata samaki hao wenye uzito wa tani 296.32 ambao maarufu kama ‘samaki wa Magufuli’ ni 115 ambazo ni za elimu vikiwemo vyuo vya juu, shule za sekondari na msingi, vyuo vya polisi, magereza, uhamiaji, hospitali, vituo vya kutunzia watoto yatima, kambi za wazee, na makanisa na misikiti inayohifadhi watoto yatima.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli alisema samaki hao wataanza kuwagawa katika eneo la Kampuni ya Bahari Foods Limited iliyopo Mwenge, Dar es Salaam walikohifadhiwa kwa gharama ya Sh milioni 800 tangu wakamatwe. Samaki hao waliokamatwa Machi mwaka huu, wa chini ana uzito wa kilo 25 na wa juu ana kilo 300.
Magufuli alisema kutokana na kukamatwa kwa samaki hao wenye thamani ya Sh bilioni mbili pamoja na juhudi za serikali za kuzuia uvuvi haramu “sasa mataifa mbalimbali yameanza kutuandikia wakitaka kuja kuvua kihalali”.
Akizungumzia makubaliano waliyofikia nchi za Kenya, Tanzania na Uganda Novemba mwaka huu juu ya kuzuia uvuvi haramu katika ziwa Victoria, alisema kila nchi itatoa Dola za Marekani 600,000 kwa ajili ya kuendesha operesheni maalumu na kusisitiza “operesheni hiyo lazima ifanyike kabla ya Januari 2010”.
Alisema operesheni hiyo imekuja baada ya uchunguzi kubainisha samaki hasa sangara katika ziwa Victoria wamepungua. Wamepungua kutoka tani milioni 1.2 mwaka 2000 hadi 310,000 Agosti mwaka huu.
“Hata hivyo, kidogo sangara wameongezeka kwani Agosti mwaka jana walikuwa tani 227,000 na tunaelezwa kuwa soko kubwa lipo DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) ambapo wanapitia Uganda. Kutokana na kupungua huko kumesababisha viwanda vitano vya Afrika Mashariki kufungwa na vilivyobaki kuzalisha chini ya uwezo kwa asilimia 60,” alisema Magufuli. Source gazeti la Mwananchi la leo.
Comments