Monday, November 16, 2009

Kikwete: Wazee hawana nafasi 2010


Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa kama akijaliwa kupata kipindi cha pili cha kuliongoza taifa la Tanzania, atafanya jitihada kubwa kuubadilisha uongozi wa Tanzania kuwa uongozi wa vijana.

Rais Kikwete pia amesema kuwa vijana ndiyo Tanzania ya kesho, na kama Tanzania haikuwekeza vya kutosha katika vijana na maendeleo yao, basi itakuwa haiwekezi katika hali yake ya baadaye.

Akizungumza jana mjini Dar Es Salaam na vijana kutoka nchi mbali mbali za Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa Kulea Uongozi wa Afrika wa African Leadership Initiative, Rais Kikwete amesema kuwa anauthamini Mpango huo.

Amewaambia vijana hao ambao wanashiriki katika Mpango huo unaodhaminiwa na Askofu Mkuu (mstaafu) wa Kanisa la Anglikan Desmond Tutu wa Afrika Kusini kuwa kwa kadri miaka inavyokwenda ni lazima rika la wazee lipishe lile la vijana.

Rais amewaambia vijana hao kwenye mkutano wao katika Hoteli ya Southern Sun mjini Dar Es Salaam: “Kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, kama nitajaliwa na nikapata bahati ya kuchaguliwa tena, nitahakikisha kuwa naubadilisha uongozi wa Tanzania kwa kuufanya uongozi wa vijana zaidi.”

Ameongeza: “Wale viongozi wa rika langu lazima waanze kuwaachia nafasi vijana. Tunahitaji wakuu wa wilaya vijana zaidi, wakuu wa mikoa vijana zaidi, na hata mawaziri vijana zaidi. Ndivyo ilivyotokea kwetu sisi wakati tukiwa vijana.”

Amesisitiza: “Vijana ndiyo matumaini ya nchi hii katika miaka inayokuja, na kama hatukuwekeza katika vijana wetu, basi ni dhahiri kuwa hatuwekezi ipasavyo katika miaka ijayo ya taifa letu.”

Akijibu maswali ya vijana hao kutoka nchi mbali mbali za Afrika zikiwamo Tanzania, Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uganda, Rais Kikwete amewaeleza vijana hao jinsi gani alivyojikuta anaingia katika siasa.

Akijibu swali kuhusu maendeleo ya karibuni katika siasa za Zanzibar, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba vyama vya siasa katika Zanzibar vimeamua kuachana na siasa na mazoezi ya zamani na kuanza ukurasa mpya. Taarifa ya Ikulu Press ya leo.

No comments: