Ugawaji samaki wa Magufuli wakwama



UGAWAJI wa tani 296.32 za samaki waliovuliwa kwa njia haramu katika ukanda wa Tanzania kwenye Bahari ya Hindi uliopangwa kufanyika jana, umekwama.

Samaki hao maarufu kama 'Samaki wa Magufuli', hawakugawiwa jana kwa taasisi zilizoteuliwa kupata mgawo kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana.

Kazi ya kugawa samaki hao ilipangwa kufanyika jana jijini Dar es Salaam katika kiwanda cha kuhifadhia samaki cha Bahari Foods kilichopo Mwenge.

Hata hivyo, utata uligubika kazi hiyo na kuifanya ishindiane na serikali haikutoa ufafanuzi kuhusu kukwama kwa zoezi hilo.

Majira ya saa 4.00 waandishi wa habari na baadhi ya wananchi walifika katika kiwanda cha Bahari Foods wakisubiri zoezi la ugawaji wa samaki hao lianze, lakini muda ulipita bila matumaini ya kuwaona samaki hao zaidi ya taarifa kutoka kwa walinzi wa kiwanda hicho kueleza kuwa zoezi hilo limesitishwa hadi litakapopangiwa siku nyingine.

Juhudi za kuwapata viongozi wa ngazi za juu akiwemo Waziri John Magufuli, katibu wa rasilimali za bahari, Gefrey Nanyalo, na viongozi wengine hazikuweza kufanikiwa.

Baadhi ya maafisa wa wizara hiyo, ambao kwenye majengo ya ofisi za wizara hiyo, walisema hawakuwa na taarifa rasmi kuhusu zoezi hilo zaidi ya kudai kutakiwa kusubiri taarifa kutoka ngazi za juu yao.

Walisema taarifa walizonazo juu ya kusitishwa zoezi hilo ambazo si rasmi ni kwamba wizara ilikosa vifaa vya kukatia samaki hao, lakini wadau walihoji sababu za wizara kutangaza zoezi hilo bila ya maandalizi.

“Mimi mwenyewe nilijua leo tunakwenda kwenye ugawaji samaki lakini muda si mrefu ndiyo nimepokea taarifa zikinieleza kuwa zoezi limesitishwa na litapangiwa muda mwingine, lakini sababu zaidi bado hazijatolewa ingawa za awali nimeelezwa kuwa ukosefu wa vifaa mbalimbali vya kukatia samaki hao ndiyo umekwamisha zoezi hilo,’’ alisema mmoja wa maafisa wa wizara hiyo. Imeandikwa na Festo Polea na Tumsifu Sanga.

Comments