Sunday, November 15, 2009

Mo Ibrahim: Viongozi Afrika si makini




MMILIKI wa taasisi ya Mo Ibrahim amesema matatizo yote yanayoikumba nchi za bara la Afrika, ikiwemo vita, njaa na magonjwa, yanatokana na viongozi wake kutokuwa makini na kutofuata misingi ya utawala bora.
“Viongozi wetu wengi si makini na pia hawafuati misingi ya utawala bora na kutokana na haya ndio maana bara hili bado lipo nyuma kiuchumi na linasumbuliwa na matatizo ya njaa, magonjwa na vita,” alisema mmiliki huyo, Mo Ibrahim jijini Dar es Salaam juzi katika hafla maalum ya muziki ikiwa ni sehemu ya maadalizi ya mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Milimani City.
Katika mkutano uliokutanisha viongozi mbalimbali kutoka nchi za bara la Afrika, pamoja na mambo mengine walijadili masuala mbalimbali yakiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa, kilimo na maendeleo ya nchi za Afrika.
Mo Ibrahim, ambaye ni milionea alifafanua kwamba viongozi wa nchi za Afrika ni wepesi wa kuzungumza lakini si watendaji katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.
Alisema kutokana na hali hiyo, Afrika inaonekana ni bara masikini na lenye matatizo mengi ikiwa ni pamoja na vita, njaa na magonjwa. Imeandikwa na Sadick Mtulya.

No comments: