Mengi's Press Conference

Leo Mzee Mengi kakutana na waandishi wa habari (dakika chache zilizopita) na hiki ndicho alichoongea:

TAARIFA YA MWENYEKITI MTENDAJI WA IPP LTD. BW. REGINALD A. MENGI KWA VYOMBO VYA HABARI
6 NOVEMBA, 2009

_____________________________________________


Ndugu Waandishi wa habari,

Nimewaita hapa leo kuzungumza nanyi kwa lengo la kuweka rekodi sawa.

Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikituhumiwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba mimi si Mwanachama wa Chama hicho na kwamba sitoi misaada ya hali na mali kwa Chama Cha Mapinduzi.

Ndugu Wanahabari,

Kwa msemo wa kiingereza “Don’t argue with a fool because people may not know the difference between you and the fool”, wenye maana kwamba usibishane na mjinga kwa sababu watu wanaweza kushindwa kufahamu tofauti yako na huyo mjinga!

Hata hivyo wakati mwingine inakulazimu kujibu hoja unapomwona mtu anapotosha mambo kwa makusudi.

Kwanza, kuhusu kuropoka kwamba sitoi misaada kwa CCM, hilo ni jambo linalozushwa na watu binafsi na kwa malengo binafsi. Viongozi wakuu wa CCM ambao ni waadilifu na wanaosimamia ukweli wanajua undani wa jambo hili.

Pili, kuhusu uwanachama wangu wa CCM:

Napenda kuwaambia kwamba mimi ni Mwanachama wa CCM tangu tarehe 18 Aprili,1977 na kadi yangu ni Na. B124595, iliyotolewa na Tawi la Kisutu, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.

Hivyo basi madai yote kwamba mimi si mwanachama au nilijiunga na chama hivi majuzi kama inavyoelezwa na Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora Sophia Simba, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Kilumbe Ng’enda na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa DSM John Guninita ni uongo, uzushi na umbea wenye lengo la kudhoofisha juhudi za viongozi wa juu wa CCM na baadhi ya wanachama za kupiga ufisadi vita.

Mimi na wenzangu wengine tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba chama chetu kinaongozwa katika misingi yake ya asili ya kupiga vita rushwa na maovu mengine.

Ndugu Wanahabari,

Hawa wanaodai kuwa ndani ya CCM hakuna kiongozi msafi ni wazi kwamba wamedandia chama hiki hivi majuzi. Ningetoa ushauri kuwa waondoke na watuachie chama chetu kwa kuwa hawafahamu msingi imara wa CCM.

Mwisho napenda kumshauri Waziri Sophia Simba kwamba katika vita dhidi ya ufisadi ni vyema akanyamaza. Kwa sababu yeye si mwadilifu na hivyo hawezi kusimama kupinga vita ya ufisadi.

Aidha, ningemshauri kabla hajazungumza aombe ushauri kutoka taasisi za serikali kama vile usalama wa taifa badala ya kuropoka na kupotosha ukweli wa mambo.

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.


Reginald A. Mengi

MWENYEKITI MTENDAJI, IPP LTD.
__________________

Comments

John Mwaipopo said…
ngoma inogile. natafuta viza sasa.
Anonymous said…
kwani kuwa mwana CCM ndiyo inakufanya uwe mtanzania zaidi ama ni kitu gani? Jamani mbona hatuambiani ukweli na nchi hii yetu sote??
Sisi tuiso na chama chochote kile tunahakikishiwa vipi haki zetu ??

Popular posts from this blog

JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJADILIANA NA NHC NAMNA YA KUENDELEZA MAKAZI MAKAO MAKUU DODOMA

Baraza Jipya la Mawaziri