Zombe: DPP alinifanyia mchezo mchafu

MSHITAKIWA wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe ameieleza Mahakama Kuu kuwa kilichomfanya akamwaga machozi kizimbani jana ni mchezo mchafu alifanyiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Zombe ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam alijikuta akimwaga machozi mara kadhaa juzi wakati akijitetea mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Masatti kuhusiana na tuhuma hizo zinazomkabili yeye pamoja na askari wenzake tisa.

Akijibu maswali kutoka kwa Waendesha Mashtaka(PP) jana kuhusiana na ushahidi wake wa utetezi alioutoa mahakamani hapo juzi, Zombe aliiambia mahakama kuwa maelezo yaliyoandikwa na baadhi ya washtakiwa wakiwa mahabusu, ambayo ndio DDP aliyatumia kama ushahidi wa kumuunganisha katika kesi hiyo yaliandaliwa na DPP mwenyewe na kuwapa washitakiwa hao.

Zomba alisema kutokana na maelezo hayo kupangwa yalitolewa gerezani hapo kwenda kwa DPP kwa njia za panya bila kupitia kwa Mkuu wa Gereza la Ukonga wanaohifadhiwa, kama utaratibu ulivyo.

Alidai kuwa barua za maelezo ya washitakiwa hao zote ambazo nakala zake alizitoa juzi mahakamani hapo kama vielelezo kwa ajili ya ushahidi wake yaliandikwa Juni 3 mwaka 2006 mchana ingawa baadhi hazina tarehe.

Comments