Hatima ya Zombe J'3




AKIJIBU AU ASIPOJIBU ATAKUTWA NA HATIA
HATIMA ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili pamoja na askari wenzake 12, itajulikana Jumatatu ijayo.

Zombe, aliyekuwa mkuu wa upelelezi mkoani Dar es Salaam, RCO, na kaimu kamanda wa polisi, ARPC, wakati wa mauaji hayo ya wafanyabiashara wanne wa mjini Mahenge mkoani Morogoro na dereva mmoja wa teksi wa Manzese jijini Dar es salaam, ndiye mtuhumiwa namba moja kwenye kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu.

Wanasheria wamekuwa wakiwasilisha hoja zao kama Zombe na wenzake, wana kesi ya kujibu katika hatua za awali za kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, na baada ya mawakili wa watuhumiwa kuiambia mahakama kuwa wateja wao hawana kesi ya kujibu na hoja hizo kujibiwa jana na mawakili wa upande wa mashtaka, hukumu ya suala hilo sasa itatolewa Februari 9.

Akiahirisha kesi hiyo jana baada ya upande wa mashtaka kumaliza kujibu hoja za upande wa utetezi, jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati alisema kuwa uamuzi huo utatolewa Jumatatu saa 4:00 asubuhi.

Comments