HARARE, Zimbabwe
KIONGOZI wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai ameapishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu na hivyo kuungana na Rais Robert Mugabe katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Tsvangirai aliapishwa rasmi na Rais Mugabe jana, huku watu wachache wakiamini kuwa Tsvangirai ataweza kutekeleza mapendekezo yake mbele ya Mugabe.
Kiongozi huyo wa upinzani kupitia MDC alisema awali kuwa, anatambua kitisho cha kumezwa na chama cha Zanu-PF kama mahasimu wa zamani wa Mugabe, bila ya kubadilisha mkondo unaofuatwa na taifa linalosambaratika, kwani Tsvangirai si kiongozi wa serikali mpya ya mpito.
Pamoja na Tsvangirai manaibu waziri mkuu wawili pia waliapishwa, ambao ni Thokozani Khupe ambaye ni msaidizi wa Tsvangirai kwenye chama cha MDC na Arthur Mutambara ambaye ni kiongozi wa kundi lililojitenga kutoka MDC.
Jumanne wiki hii Tsvangirai alimteua Katibu Mkuu wa chama chake, Tendai Biti kushika wadhifa wa Waziri wa Fedha, baada ya Jaji wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo kufuta mashtaka ya uhaini dhidi yake wiki iliyopita.
Kufuatia kuapishwa kwake, Tsvangirai ana haki ya kutoa mapendekezo na wakati mwingine kumwakilisha Mugabe anayebakia kuwa rais, licha ya kushindwa uchaguzi uliofanywa mwezi wa Machi mwaka jana.
Mugabe anaendelea kuwa kiongozi wa serikali na vile vile mkuu wa Tsvangirai, hatua hiyo inaonekana kuwatia wasiwasi Wazimbabwe wengi, ambapo mmoja wao ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu, Tsitsi Torongo mwenye miaka 29 alisema:
"Mimi binafsi kamwe sijawahi kukiamini chama cha Zanu-PF. Hofu yangu ni kuwa wataendelea kuizuia serikali hiyo kufanya kazi yake na hivyo kuzuia masuala muhimu kushughulikiwa kama ipasavyo."
Comments