Watu 100 wateketea kwa moto Kenya






ZAIDI ya watu 100 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa baada ya lori la mafuta ya petroli kupinduka na kulipuka katika mji wa Molo kwenye mkoa wa Rift Valley nchini Kenya.
Taarifa kufikia jana jioni zilieleza kuwa vifo vinavyotokana na tukio hilo vilifikia 111, likiwa ni tukio la pili la moto kubwa kwa wiki hii, baada ya kuungua duka la kujihudumia vyakula na bidhaa (Supermarket) la Nakumat Downtown, Jumatano wiki iliyopita.
Katika tukio hilo la awali, zaidi ya watu 50 walipotea wakiwa hawajulikani waliko, lakini siku mbili baadaye miili ya watu 27 ikiwa imepatikana katika mabaki ya jengo la duka hilo huku juhudi za kutafuta miili zaidi zikiendelea, mingi kati ya iliyopatikana ikiwa imeteketea kiasi cha kutotambulika.
Taarifa za awali zilizotolewa jana zilieleza kuwa lori hilo la mafuta lilipoteza mwelekeo na kuacha barabara karibu na mji wa Molo ambapo mamia ya watu walijitokeza na kulizunguka lori kwa lengo la kuchota mafuta yaliyokuwa yakimwagika.
Waathirika wa ajali hiyo walikuwa wamelazwa kwenye sakafu ya hiospitali, huku wakiwa wamewekewa chupa za maji.
Ajali hiyo inadhaniwa kuwa ilitokana na mmoja wao wananchi hao wanadaiwa kuwa walikuwa wanaiba mafuta, kuwasha sigara katika eneo hilo.

Comments