Wednesday, February 04, 2009

Mawakili wasema Zombe hana cha kujibu



MAWAKILI wa washitakiwa wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, jana waliisihi mahakama kuu kuwaachia huru washtakiwa wao kwa madai katika ushahidi uliotolewa unaonyesha hawana kesi ya kujibu.

Wakitoa hoja zao za kuishawishi mahakama kuamini kuwa washtakiwa hao hawana kesi ya kujibu, mawakili hao kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama hiyo kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hauwahusishi na tuhuma za mauaji hayo moja kwa moja na badala yake ni ushahidi wa mazingira tu.

Mawakili hao pia waliuchambua ushahidi uliotolewa dhidi ya wateja wao na kuieleza mahakama kuwa unajichanganya kwa maelezo kuwa mashahidi hao wamekuwa wakipingana katika maelezo yao, jambo ambalo mawakili hao walisema linaacha utata kwa mahakama kujua ushahidi upi ni wa kweli na upi si wa kweli.

Mawakili wa washtakiwa wote waliieleza mahakama kuwa kati ya watu 37 waliotoa ushahidi mahakamani hapo, hakuna shahidi hata mmoja aliyeweza kuithibitishia mahakama hiyo jinsi washtakiwa hao walivyotenda kosa la mauaji hayo.

Walisema ushahidi wote uliotolewa ni wa kusikia tu na si wa kushuhudia kosa likitendeka. na James Magai

No comments: