MAMIA ya watu wengi wao wakiwa ni wamasai toka Simanjiro jana walimiminika katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha kufuatilia kesi ya inayomkabili mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoa wa Manyara, Christopher Ole Sendeka aliyepandishwa tena kizimbani kujibu shitaka la kumshambulia Mwenyekiti wa jumuiya ya vijana ya CCM mkoa wa Arusha, James Ole Millya.
Kesi hiyo ya jinai namba 3/2009 ambayo ilihudhuriwa na mamia ya watu wengi wao wakiwa ni wamasai toka Simanjiro, ilitajwa mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa Arusha, James Karayemaha kwa mara ya pili.
Sendeka anatuhumiwa kumchambulia Millya, Januari tisa wilayani Monduli mkoani Arusha, ambapo wote walikuwa wakihudhuria semina ya wazee wa mila ya kimasai na viongozi toka jamii ya kimasai, mkutano uliandaliwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Katika kesi hiyo jana kwa mara ya kwanza, Mawakili wawili Kelvin Kwagirwa toka kampuni ya uwakili ya Oljale na Moses Mahuma toka kampuni ya uwakili na Dancon Oola, walijitambulisha kumwakilisha Mlalamikaji James Millya.
Mawakili hao, waliomba kufuatilia kesi hiyo kwa kuwa mshitakiwa anawakilishwa na jamhuri katika shauri hilo.
Comments