Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda umefungwa rasmi jijini Kigali leo tarehe 26 Julai 2025, baada ya mawaziri wa pande zote mbili kusaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano ikiwemo ya kilimo na uanzishwaji wa Ofisi ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) jijini Kigali, kama sehemu ya hatua za kuimarisha uhusiano wa karibu na kukuza maendeleo ya pamoja baina ya nchi hizo mbili.
Hati hizo zimesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Olivier Nduhungirehe ikilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Rwanda kwa manufaa ya wananchi wa mataifa haya mawili. Kupitia makubaliano ya sekta ya kilimo, pande zote zimekusudia kubadilishana uzoefu, teknolojia, utaalamu na taarifa muhimu ili kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula na fursa za biashara ya mazao ya kilimo.
Aidha, uanzishwaji wa Ofisi ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) jijini Kigali unalenga Kurahisisha upatikanaji wa huduma za Bandari nchini Rwanda, kupunguza gharama za bidhaa, kuimarisha na kuongeza matumizi ya Bandari za Tanzania kama lango kuu ka kupitisha mizigo na shehena za Rwanda
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mkutano, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo na kuwataka wataalamu na viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa mipango na maazimio ya JPC yanatekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri Nduhungirehe ameipongeza Tanzania kwa ushirikiano mzuri na kusisitiza kuwa Rwanda itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi jirani ili kuhakikisha maridhiano ya kweli yanapatikana kupitia utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa. Ameeleza kuwa makubaliano kama hayo ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi, kuboresha usalama wa chakula, na kuimarisha mshikamano wa kidiplomasia na kijamii kati ya mataifa hayo mawili.
Mkutano wa 16 wa JPC umejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara, ulinzi na usalama, miundombinu, afya, elimu, nishati, na kilimo. Mazungumzo hayo yamekuwa na tija kubwa na kufanikisha hatua za pamoja za kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi baina ya Tanzania na Rwanda.
No comments:
Post a Comment