#Kukamilika kwa daraja wilayani Manyoni kusaidia usafirishaji wa Samaki na Chumvi
Singida
Kamati ya Ukaguzi ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ikiongozwa na Mwenyekiti wake CPA Ally Rashid imeanza ziara ya kukagua Miradi ya ujenzi wa Miundombinu ya barabara mkoani Singida.
Kamati hiyo Mkoani Singida imetembelea miradi miwili ya ujenzi wa daraja la mawe Mkonjigwe lenye urefu wa mita 42 linalojengwa katika barabara ya Chibumagwa-Sasajila-Makasuku-Itetema Kata ya Sasajila Wilayani Manyoni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mandewa 69 yenye urefu wa Km. 0.89 kwa kiwango cha lami inayojengwa katika Manispaa ya Singida.
Akielezea hali ya utekelezaji wa miradi hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema kuwa mradi wa daraja la mawe umetekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilihusisha uchimbaji wa msingi wa daraja, ujenzi wa msingi wa daraja yaani 'Raft Foundation' na nguzo za daraja.
Awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa ukuta nusu duara, mabawa ya daraja, kingo kwenye maingilio ya daraja na eneo la kutokea, ujenzi wa kuta za mawe kwaajili ya kuunganisha nusu duara, kujaza kifusi, kupanga mawe, kumwaga jamvi eneo la juu la daraja na kuchonga barabara za maingilio ya daraja.
Akielezea umuhimu wa daraja hilo kiuchumi na kijamii Mhandisi Kibasa amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa samaki, chumvi na nafaka ndani ya Wilaya ya Manyoni na kupunguza vifo vya wananchi vinavyotokana na maji wakati wa kuvuka mto hususani majira ya mvua.
Kwa upande wa hali utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mandewa 69 Mhandisi Kibasa ameeleza kuwa mpaka sasa Mkandarasi anametekeleza kazi Kwa asilimia 88 na kwa sasa anaendelea na kazi ya ujenzi wa vivuko vya magari na watembea kwa miguu na mradi huo unatarajia kukamilika tarehe 31/7/2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA Ally Rashid amesema kuwa wao wameona utekelezaji wa kazi hizo na ndio lengo la ziara yao na kuishauri TARURA Mkoa wa Singida kuendelea kusimamia Miradi hiyo ili iweze kutekelezwa kwa kuzingatia ubora sambamba na kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wa miundombinu hiyo.
No comments:
Post a Comment