Arusha, Julai 18, 2025 – Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, ameongoza hafla ya kumuapisha rasmi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Bi. Cecilia Mtanga, iliyofanyika leo katika Makao Makuu ya Shirika hilo, Mtaa wa Majengo, jijini Arusha.
Uapisho huo unafuatia uteuzi wa Kamishna Mtanga uliofanywa na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA katika kikao chake cha 210 kilichofanyika Mei 2025 jijini Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Kuji alimpongeza Kamishna Mtanga kwa uteuzi huo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya pamoja na nafasi yake ya Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu TANAPA. Alisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa watumishi wote wa Shirika katika kutekeleza dhamira ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili kwa weledi, uwajibikaji na moyo wa kizalendo kwa manufaa ya Taifa.
“Tunahitaji mshikamano na uwajibikaji ili kuhakikisha malengo ya TANAPA yanafikiwa kwa manufaa ya Taifa,” alisema Kamishna Kuji.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Cecilia Mtanga aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo. Aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa bidii, ushirikiano na kuendeleza dhamira ya Shirika katika kulinda urithi wa taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na wenzangu kuhakikisha urithi wa taifa unasimamiwa ipasavyo,” alisema Kamishna Mtanga.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi na watumishi mbalimbali wa TANAPA.
No comments:
Post a Comment