BENKI
ya NMB kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),
wamezindua mashirikiano ya kimkakati na ya Kidijitali ya Ununuzi na
Uuzaji wa Hisa za Kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa DSE ambapo kupitia
aplikesheni ya NMB mkononi unaeza kuipata huduma ya uuzaji na ununuzi
wa hisa ya DSE.
Mashirikiano
haya ni matokeo ya ubunifu na ushirikiano wa muda mrefu kati ya NMB na
DSE, uliounganisha rasmi mifumo miwili ya suluhishi za kidijitali za NMB
Mkononi ya Benki ya NMB na Hisa Kiganjani ya Soko la Hisa Dar es
Salaam.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Afisa
Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema wanajivunia mashirikiano
mema na DSE, yaliyozaa huduma hiyo inayowapa Watanzania na Wawekezaji
wengine njia rahisi, salama na za kisasa za kushiriki uwekezaji.
“Huduma
hii ya Ununuzi na Uuzaji wa Hisa kupitia NMB Mkononi, ni matokeo ya
Ubunifu na Ushirikiano baina ya NMB na DSE, uliounganisha mifumo ya NMB
Mkononi na Hisa Kiganjani, bunifu na kazi kubwa iliyowezeshwa kwa juhudi
za wataalamu wa TEHAMA kutoka pande zote mbili.
“Kupitia
huduma hii tunayozindua leo, wateja wa NMB sasa wataweza kujisajili,
kununua, kuuza hisa na kufanya malipo kupitia akaunti za NMB, kupata
taarifa ya thamani ya uwekezaji wao, kuona bei za hisa zilizoorodheshwa
DSE na kujua mwenendo wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.
“Hili
ni jukwaa linaloenda kuleta mapinduzi ya kweli katika ushiriki wa
Watanzania kwenye Sekta ya Fedha, hususani Masoko ya Mitaji na Dhamana,
lakini pia ni kielezo na uthibitisho wa dhamira ya dhati ya NMB
kuwezesha ushirikishwaji wa kifedha kwa njia ya teknolojia,” alibainisha
Bi. Zaipuna.
Akizindua
huduma hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,
Profesa Kitila Mkumbo, alizipongeza NMB na DSE kwa ubunifu wa kiwango
cha juu, unaoenda kuisadia Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dk. Samia
Suluhu Hassan katika maeneo makuu manne muhimu kiuchumi.
Aliyataja
maeneo hayo aliyosema yamo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo, kuwa ni
pamoja na Kuimarisha Upatikanaji wa Huduma kwa Wananchi, Kusaidia
Kubadili Mitazamo ya Wananchi, Kuelimish Jamii Juu ya Uwekezaji na
Kuchagiza Ushirikiano kwa Taasisi za Ndani.
“Hili
linalofanyika hapa ni tukio zuri na la maana sana, pongezi kwa NMB na
DSE kwa huduma hii, kwetu sisi kama Serikali, hili ni jambo kubwa,
muhimu na la maana sana linaloenda kutusaidia katika maeneo makuu manne
ambayo ni muhimu kwa ustawi na ukuaji wa kiuchumi.
“Moja,
huduma hii inaenda kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,
Serikali na Chama Tawala tunayo Mpango wa Maendeleo wa Taifa, ambao
unataka ifikapo mwaka 2030, huduma zote za Kiserikali zimfikie mwananchi
popote alipo, hili mnalozindua leo, mmetutangulia sana.
“Pili,
mnaenda kusaidia kubadili mitazamo ya wananchi walio wengi. DSE ni
kongwe, ilipoanza ilikuwa ngumu kumwambia Mtanzania anunue Hisa, sasa
hii huduma inaenda kubadili mitazamo ya Watanzania juu ya Hisa, kwamba
Utajiri sio tu kuwa na magari, majumba na viwanda, bali hata Hisa ni
Utajiri pia.
“Pia
katika eneo la tatu, huduma hii itakuza uelewa katika suala zima la
uwekezaji. Kwa kweli huduma hii inaenda kuchochea uwekezaji miongoni mwa
Watanzania. Inaenda kubadili mitazamo hasi juu ya uwekezaji kwamba sio
kwa ajili ya wageni tu, bali hata wazawa wanapaswa na wanaweza kuwekeza.
“Ili
uchumi ukue, watu wanahitaji kuwekeza na hatua ya kwanza ni uwekaji
akiba, ili akiba izae, ndio linapokuja suala na ununuzi wa hisa, ambao
unafaida kubwa. Eneo la nne ni ushirikiano mliokuja nao NMB na DSE. Ni
taasisi za ndani zenye mafanikio na mnapokuja na aina hii ya
ushirikiano, mnachagiza wengine,” alibainisha Profesa Kitila.
Naye
Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, alisema wao wanajisikia
fahari sio tu kwa kuwa sehemu ya mashirikiano ya muda mrefu na NMB, bali
ufanikishaji wa uzinduzi wa huduma bora ya kidijitali inayoenda kutanua
wigo wa ushiriki wa Watanzania katika masuala mazima ya uwekezaji kwa
njia ya hisa.
“NMB
ni taasii inayoaminika, kinara wa ushirikiashaji jamii katika Huduma
Jumuishi za Kifedha kwa Watanzania wa kadfa zote, ushirikiano huu na
huduma hii ni uthibitisho kuwa taasisi hizi mbili zina dhamira ya dhati
ya kukuza maslahi na ustawi wa wananchi.
“Wito
wetu kwa umma hasa vijana, wawekeze sio kwa sababu wana pesa nyingi,
bali kwa sababu wanahitaji kuwa na kesho iliyo bora na sisi kwa upande
wetu, tunapambana kuondoa dhana hasi kuwa uwekezaji ni lazima uwe na
mabilioni ya fedha, bali kwa kiasi chochote unaweza kuanza nacho
uwekezaji,” alisema Nalitolela.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Soko la Mitaji
na Dhamana (CMSA), CPA Alfred Mkombo, akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu
wa CMSA, Nicodemus Mkama, aliitaja huduma hiyo kuwa ni hatua muhimu
katika Sekta ya Fedha, hasa Soko la Mitaji na Dhamana nchini.
“Sisi
CMSA tukiwa wasimamizi wa mitaji, tuna jukumu la kusimamia huduma zote
za Masoko ya Mitaji, tunapongeza jitihada hizi za NMB na DSE kwa sababu
ubunifu wao unaenda kutanua wigo wa Masoko ya Mitaji kuyafikia makundi
yaliyoachwa nyuma katika hili.
“Hudum
hii inayozinduliwa leo inaenda kuwa chachu ya wananchi wote kushiriki
katika fursa za uwekezaji mijini na vijijini, hasa ukizingatia kuwa NMB
Mkononi ina mtandao mpana unaojumuiosha wateja zaidi ya milioni 7 wa
kada tofauti kote nchini.
“Tunazipongeza
Bodi za NMB na DSE kwa ushirikiano huu unaozinda huduma hii iliyokidhi
mahitaji na matakwa ya kikanuni ya CMSA,” alisisitiza Mkombo mbele ya
waalikwa wa hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Msajili wa Baraza la Soko
la Mitaji na Dhamana, Martin Kolikoli.
No comments:
Post a Comment