Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 30 Julai 2025, ameandika historia mpya kwa kuzindua rasmi usafirishaji wa mizigo kwa kutumia Treni ya Umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kupitia Kituo cha Kwala, mkoani Pwani.
Uzinduzi huu ni hatua kubwa ya maendeleo katika sekta ya uchukuzi, ukilenga kuboresha usafirishaji wa mizigo nchini kwa kutumia miundombinu ya kisasa, rafiki kwa mazingira na yenye kasi zaidi. Treni hii ya umeme inatarajiwa kupunguza muda wa kusafirisha mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji, pamoja na kupunguza msongamano wa malori barabarani.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Mhe. Rais Samia amesema kuwa utekelezaji wa mradi huu mkubwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo Afrika Mashariki na Kati.
“SGR ni mradi wa kimkakati. Leo tunashuhudia ndoto kubwa ya Watanzania ikitimia – mizigo sasa inasafirishwa kwa haraka, salama na kwa tija zaidi,” alisema Rais Samia.
Treni hiyo ya umeme inatarajiwa kuongeza ufanisi katika usambazaji wa bidhaa, kusaidia wakulima, wafanyabiashara na viwanda kwa kusafirisha bidhaa kwa bei nafuu na kwa wakati.
No comments:
Post a Comment