Dodoma, 28 Julai 2025 – Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kilichofanyika jijini Dodoma kwa madhumuni ya kujadili masuala muhimu ya chama na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Kikao hicho cha juu cha uongozi wa CCM kimewakutanisha viongozi hao waandamizi wa chama kujadili majina ya watia nia. Aidha, kikao hicho kimeangazia pia mipango ya chama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa chama kuendelea kuwa karibu na wananchi, kuhakikisha utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni unaendelea kwa kasi na ufanisi. Amesisitiza pia dhamira ya chama kuendeleza utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na maendeleo jumuishi.
“Ni wajibu wetu kama viongozi wa CCM kuhakikisha kuwa tunasimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi, kwa kuwa ndiyo mkataba kati ya chama na wananchi. Tunatakiwa kuwa na chama kinachoishi na kuishi na watu,” alisema Mhe. Dkt. Samia.
Viongozi mbalimbali waliotoa michango yao katika kikao hicho wameelezea mafanikio ya Serikali chini ya uongozi wa CCM, huku wakipendekeza maeneo ya kuboresha zaidi huduma za jamii, miundombinu, elimu, afya na uwezeshaji wa vijana na wanawake.
Kikao hiki cha Kamati Kuu ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya ndani ya chama inayolenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya CCM kama chama tawala, pamoja na kuhakikisha kuwa masuala ya msingi yanashughulikiwa kwa mujibu wa dira na misingi ya chama.
Mwisho wa kikao, wajumbe walieleza kuridhishwa na maelekezo ya Mwenyekiti na kuweka mikakati ya pamoja ya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa.
No comments:
Post a Comment