Dar es Salaam, 6 Julai 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametembelea banda la Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Dkt. Abbas amepongeza juhudi na ubunifu unaoonyeshwa na TANAPA katika kutangaza vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji, pamoja na juhudi za kuhamasisha uhifadhi endelevu wa maliasili na wanyamapori wa Taifa. Amesema kuwa muonekano wa banda hilo na umahiri wa maafisa wake katika kutoa elimu kwa wageni ni ishara ya utayari wa taasisi hiyo kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kupitia utalii wa hifadhi.
“Mmenipendeza sana. Banda lenu limekuwa moja ya vivutio vikubwa katika maonesho haya, na muamko wa wadau na wananchi waliotembelea hapa ni wa kutia moyo. Hii ni dalili kwamba kazi yenu ya kuelimisha, kuhifadhi, na kutangaza vivutio vya asili inaungwa mkono na jamii,” alisema Dkt. Abbas.
Aidha, Katibu Mkuu ameeleza kufurahishwa na ushindi wa tuzo saba za kimataifa za utalii ambazo TANAPA imepata katika kipindi kifupi, na kuitaka taasisi hiyo kuendeleza jitihada hizo ili kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kinara wa utalii barani Afrika. Alisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za asili kwa uangalifu mkubwa ili ziweze kuendelea kuchangia uchumi wa Taifa kupitia utalii wa ndani na wa kimataifa.
“Tunapopata tuzo nyingi kama hizi, maana yake ni kwamba dunia inatambua kazi yetu. Lakini pia tuendelee kulinda wanyamapori wetu, mito, misitu na mazingira ya asili – haya ndiyo nguzo za ustawi wa sekta ya utalii na kiuchumi kwa ujumla,” aliongeza Dkt. Abbas.
Banda la TANAPA katika maonesho ya Sabasaba mwaka huu limekuwa kivutio kwa wageni wa rika mbalimbali, likiwa na maonyesho ya video za vivutio, mabango ya kitaalamu, sampuli za mazao ya utalii, na maelezo ya fursa za uwekezaji katika hifadhi mbalimbali nchini.
TANAPA imeeleza kuwa inatumia jukwaa hili kubwa la kibiashara sio tu kutangaza hifadhi zake, bali pia kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na mchango wa sekta ya maliasili katika maendeleo ya Taifa.
Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yanaendelea hadi tarehe 13 Julai 2025 yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi zaidi ya 3,500, huku yakifanyika chini ya kaulimbiu ya mwaka huu: “Biashara Endelevu kwa Uchumi Shindani”.
No comments:
Post a Comment