Thursday, July 10, 2025

MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII ZASISITIZWA KUWEKEZA KWA UMAKINI ILI KULINDA MASLAHI YA WANACHAMA – DKT. MPANGO

















Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amezitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika miradi ya miundombinu haudhoofishi malengo ya msingi ya kuanzishwa kwake, hususan ulinzi wa kijamii na kiuchumi kwa wanachama wake.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo leo Julai 10, 2025, wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Ameeleza kuwa michango ya wanachama ni nguzo muhimu ya hifadhi dhidi ya misukosuko ya maisha, hivyo lazima ibaki kuwa salama na ya kutosha kufanikisha malengo ya hifadhi ya jamii.

Amesisitiza kuwa ni lazima kuwe na umakini mkubwa katika kuwekeza kwenye miradi ya miundombinu, kwa kuwa miradi isiyotekelezeka au iliyobuniwa vibaya inaweza kuhatarisha uwezo wa mifuko hiyo kutimiza wajibu wake kwa wanachama.

Makamu wa Rais ameeleza kuwa baadhi ya miradi imekuwa na gharama kubwa zisizokuwa na tija, changamoto katika usimamizi, au kutokidhi mahitaji ya wanufaika wa mifuko hiyo. Ameonya kuwa kutofanya upembuzi yakinifu wa kina kunaweza kusababisha kuchelewesha au kushindwa kabisa kutoa mafao kwa walengwa.

Dkt. Mpango pia ametoa wito kwa wataalamu wanaoshiriki mkutano huo kuandaa mikakati madhubuti ya kuwezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi hususan katika maeneo ya vijijini. Ameeleza kuwa uwekezaji katika maeneo hayo utaongeza tija, ubora wa maisha, ajira na kupunguza wimbi la uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, upungufu wa kila mwaka wa fedha za kugharamia miundombinu Barani Afrika unakadiriwa kuwa kati ya dola za Kimarekani bilioni 68 hadi 108, hali inayotoa fursa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuchukua nafasi ya kuharakisha maendeleo ya bara hilo kwa kutoa ufadhili endelevu.

Aidha, amewahimiza watunga sera kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kutoa mapendekezo ya vitendo kuhusu jinsi mifuko hiyo inaweza kuwa chombo imara na endelevu cha kuchochea maendeleo ya miundombinu kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi na wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wakiwemo Mawaziri na Wakurugenzi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni: “Mifuko ya Hifadhi ya Jamii: Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu na Ukuaji wa Kiuchumi na Kijamii Barani Afrika.”

No comments:

WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA AMALIZA ZIARA YA SIKU MOJA MKOANI MBEYA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), leo ameondoka Mkoani Mbeya baada ya kukamilisha zi...