Moroni, Comoro – Julai 6, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bergamo uliopo mjini Moroni, Visiwa vya Comoro, kwa ziara ya kikazi ya siku moja kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani.
Mara baada ya kuwasili, Rais Dkt. Samia alilakiwa kwa heshima ya kijeshi na kukagua Gwaride la Jeshi la Umoja wa Visiwa vya Comoro, ikiwa ni sehemu ya mapokezi rasmi kwa viongozi wa kitaifa wanaoalikwa katika shughuli za kitaifa.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Samia atashiriki kama Mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Malouzini Omnisport, mjini Moroni.
Ushiriki wa Tanzania katika maadhimisho haya unaonesha kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Comoro, huku ukisisitiza dhamira ya Tanzania katika kudumisha mshikamano na udugu wa kihistoria na mataifa jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika na Bahari ya Hindi.
Rais Dkt. Samia anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Azali Assoumani kuhusu masuala ya ushirikiano wa pande mbili, hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji, utalii, elimu na afya.
Ziara hii inadhihirisha msimamo thabiti wa Tanzania wa kuendeleza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment