Dar es Salaam, 25 Julai 2025 —
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza tukio la kuweka jiwe la msingi na kukata utepe ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa Kanisa la Arise and Shine, lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo lenye uzito wa kiimani na kijamii, Mheshimiwa Rais alisogeza kitambaa kama ishara ya uwekaji rasmi wa jiwe la msingi la jengo hilo la ibada, akifuatiwa na zoezi la kukata utepe kwa heshima kubwa, kuashiria kuwa jengo hilo sasa limefunguliwa rasmi kwa matumizi ya waumini na jamii kwa ujumla.
Akizungumza na viongozi wa dini, waumini pamoja na wageni waalikwa waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, Mheshimiwa Rais Samia aliipongeza jamii ya Arise and Shine kwa dhamira yao ya kujenga nyumba ya ibada yenye hadhi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za dini kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha maadili, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
“Makanisa, misikiti na nyumba zote za ibada ni sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii. Hapa ndipo tunapojifunza kuishi kwa maadili, tunajifunza kuvumiliana, na kuombeana mema kama Taifa. Serikali yangu itaendelea kuwa bega kwa bega nanyi katika kuimarisha maisha ya kiroho sambamba na maendeleo ya kijamii,” alisema Rais Samia.
Kanisa la Arise and Shine ni mojawapo ya makanisa yanayokua kwa kasi jijini Dar es Salaam, likiwa na mkakati mpana wa kutoa huduma za kiroho, kijamii na kiuchumi kwa jamii ya Kawe na maeneo jirani. Jengo hilo jipya lina uwezo wa kuchukua waumini zaidi ya 1,000 kwa wakati mmoja, na linajumuisha pia vyumba vya shule ya Jumapili, ofisi za kiutawala, na eneo la maombi.
Tukio hilo pia lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, na wananchi waliofurika kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
No comments:
Post a Comment