Katika kuadhimisha Siku ya Kiswahili duniani, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Muungano wa Visiwa vya Comoro zimekubaliana kuendeleza mazungumzo ya kuanzisha rasmi ufundishaji wa Kiswahili katika shule za Comoro, kufuatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa walimu na vifaa vya kufundishia lugha hiyo.
Makubaliano hayo yalitangazwa rasmi na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu na Waziri wa Elimu wa Comoro, Mhe. Bacar Mvoulana, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika mjini Ntsaoueni, katika Kisiwa cha Ngazidja. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Gavana wa Kisiwa hicho, Mawaziri wa Serikali ya Comoro, Balozi Mdogo wa Afrika Kusini, wawakilishi wa taasisi za kimataifa, mashirika ya kiraia pamoja na wananchi kutoka miji 11 inayozungumza Kiswahili katika kisiwa hicho.
Akihutubia kwenye hafla hiyo, Balozi Yakubu alirejea msimamo wa Tanzania ulioelezwa na Rais Samia wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Comoro, ambapo alisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro kwa kutoa walimu na vifaa vya kujifunzia ili kufanikisha azma ya kuendeleza Kiswahili visiwani humo.
“Tanzania inaipongeza Serikali ya Comoro kwa kuonesha utayari wa kuitambua Kiswahili kama lugha rasmi na kufundishwa mashuleni. Uhusiano wa kihistoria na kiutamaduni baina ya nchi zetu unapaswa kuendelezwa kupitia lugha hii adhimu,” alisema Balozi Yakubu.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu wa Comoro, Mhe. Bacar Mvoulana, alieleza kuwa Serikali ya Comoro imepokea kwa faraja ahadi ya Tanzania na itaendelea na mchakato wa ndani wa kufanya tathmini ya mahitaji ya kitaaluma na kiutawala ili kuwezesha ufundishaji wa Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu.
Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo taarab kutoka kwa msanii mashuhuri wa Tanzania Mzee Yusuf, kikundi cha Taarab Ayn kutoka Comoro, ngoma ya asili ya Lelemama kutoka kundi la Salama Mapesa pamoja na mchezo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu. Pia mada kadhaa kuhusu nafasi na fursa za Kiswahili nchini Comoro ziliwasilishwa na wanazuoni na wadau wa lugha.
Maadhimisho haya yameonesha dhamira ya dhati ya kukuza na kueneza Kiswahili katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utambulisho wa Kiafrika na mshikamano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, ambapo Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi.
No comments:
Post a Comment