Friday, July 04, 2025

𝗪𝗔𝗡𝗔𝗡𝗖𝗛𝗜 𝗪𝗔𝗙𝗨𝗥𝗔𝗛𝗜𝗦𝗛𝗪𝗔 𝗡𝗔 𝗨𝗣𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔𝗡𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗕𝗘𝗚𝗨 𝗕𝗢𝗥𝗔 𝗭𝗔 𝗠𝗜𝗧𝗜









Dar es Salaam. Wananchi wameeleza kufurahishwa na juhudi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za miti na elimu ya uhifadhi, katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Ikiwa leo ni siku ya saba ya maonesho hayo, mamia ya wananchi wameendelea kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, hususan katika eneo la TFS, ili kupata mafunzo kuhusu uhifadhi wa misitu na ufugaji wa nyuki.

Baadhi ya wananchi wamesema kuwa wamevutiwa na namna TFS inavyowaelimisha kuhusu upandaji wa miti bora kulingana na aina ya udongo na hali ya hewa ya maeneo mbalimbali nchini

“Nimejionea miche mizuri kabisa na nimenunua mbegu na miche. Hii si mara ya kwanza kununua hapa. Kwa kweli TFS wanafanya kazi nzuri katika kuhakikisha wananchi wanapata mbegu bora za miti na elimu ya kupanda miti inayofaa kwa maeneo tofauti,” alisema Ndg. Tabu Ramadhan, mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo.

Naye Ndg. Geofrey Mati alieleza kuwa mafunzo aliyoyapata yameongeza uelewa wake kuhusu upandaji miti.

“Nimepewa elimu nzuri sana ya upandaji miti katika eneo ninaloishi. Wamenieleza kuwa si kila mti unapandwa popote; inategemea na udongo na hali ya hewa ya eneo husika. Hapo awali sikuwa nafahamu, lakini sasa nimepata uelewa mkubwa sana,” alisema Mati.

Mbali na elimu ya miche na mbegu bora, wananchi pia wamepata fursa ya kujionea shughuli za ufugaji nyuki, zikiwemo maandalizi ya manzuki, uvunaji na uchakataji wa mazao ya nyuki.

Aidha, TFS imewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda lao katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi juu ya uhifadhi wa misitu, ufugaji wa nyuki, pamoja na kupata ofa maalumu za kutembelea vivutio vya utalii wa ikolojia vinavyosimamiwa na wakala huo.

Maonesho ya Sabasaba 2025 yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, yakishirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi. 

@treeseedstz

No comments:

WANANCHI 216 WAKABIDHIWA HATI MILIKI WILAYANI MASWA

Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Simiyu, leo imeendesha zoezi la kugawa jumla ya hati miliki 216 kwa wananchi wa Wilaya ya Maswa....