Watu 20 wafa maji

ZAIDI ya watu 20 wanasadikiwa kufa maji katikati ya Bahari ya Hindi  na wengine 13 kuokolewa baada ya boti walilokuwa wakisafiria kutoka Tanga kuelekea kisiwani Pemba kushika moto.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Nyakoro Sirro, ajali hiyo ilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia jana katikati Bahari ya Hindi wakati.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema boti hiyo ambayo ni mfano wa jahazi ililopata ajali hiyo ni la kubeba mizigo linalojulikana kwa jina la ‘Amana Pemba”, ambalo hufanya safari zake kati ya Pemba ,Unguja, Dar es saalam na Tanga.

Kamanda Sirro alisema boti hilo lilikuwa na kibali cha kuondoka katika Bandari ya Tanga saa 11:00 jioni kwenda Pemba, lakini halikuondoka hadi saa 3:30 usiku ndipo likaanza safari yake ya kuelekea Pemba likiwa na mizigo na abiria 40.

Kamanda Sirro alisema kwa mujibu wa taarifa alizopata, ajali hiyo ilisababishwa na godoro ambalo lilishika moto baada ya kugusa injini na kisha kulipuka.

Alisema mmoja wa abiria waliokuwa ndani ya boti hilo aliuona moto huo akapiga
kelele na wengine wakaanza kutapatapa huku baadhi yao wakichupa majini ili kujiokoa.
 
“Abiria mmoja alitupigia simu kututaarifu juu ya tukio hilo na kuomba msaada, ndipo Boti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ikaondoka usiku huo kwenda kuwaokoa, lakini ilipofika katikati ilishindwa kuendelea na safari kutokana na mawimbi kuwa makubwa hivyo ikarejea Tanga,” alisema Sirro.taarifa ya mdau Burhan Yakub wa Mwananchi.

Comments