Wednesday, April 08, 2009

Mvua za leo nooma kweli




MVUA zilizonyesha jana jijini Dar es Salaam zilileta adha kubwa ya usafiri na kusababisha abiria kukaa vituoni kwa zaidi ya saa mbili hadi tatu wakisubiri daladala ambazo zilionekana kuwa chache.

Katikati ya jiji la Dar es Salaam maji yalikuwa yamejaa barabarani na mitaro kuonekana kuziba huku wananchi wakikanyaga maji machafu na wengine kuvua viatu ili waweze kupita huku magari madogo ya kizima katikati ya barabara kutokana na maji kuwa mengi barabarani.

Mwananchi ambalo lilizunguka katika baadhi ya maeneo ya jiji kujionea hali hiyo lilishuhudia abiria wakiwa wamesimama vituoni katika barabara ya Mwenge-Posta ambapo magari mengi yaliyokuwa yakitoka mjini yanakuwa yamejaa na yakipita kwa uchache.

Kutokana na foleni kubwa iliyokuwepo magari yalikuwa yakipita njia mbalimbali za uchochoroni ambapo nako foleni zilikuwa kubwa na kusababisha kuchukua muda wa saa mbili hadi tatu kufika Mwenge.

Katika kituo cha Ubalozi kilichopo karibu na ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam, Mwananchi lilishuhudia abiria wakiwa kituoni kwa zaidi ya saa tatu bila kupata usafiri huku daladala za Mwenge-Posta zikipita chache na zikiwa zimejaza abiria kupita kiasi.

Vivyo hivyo kwa abiria waliokuwa wakielekea Mwananyamala ambao nao walionekana kukaa vituoni kwa muda mrefu bila kupata usafiri.

Katika barabara za uchochoroni zilizopo eneo la Makumbusho foleni ilikuwa kubwa kutokana na kila mwenye gari kutafuta njia fupi ya kuweza kuepuka foleni bila kufanikiwa.

Mwananchi ambalo lilipita njia hiyo ili kukwepa foleni lilijikuta likikwama kwas zaidi ya saa moja na nusu kutokana na foleni iliyokuwepo katika vichochoro hivyo.

Katika kituo cha daladala cha Mwenge daladala za kwenda Mikoroshini na Veternary ziliokuwa chache kiasi cha kufanya abiria kuwa wengi kituoni bila kupatikana kwa usafiri huku mvua ikinyesha kubwa.

No comments: