Mzee Kabuye afariki dunia
Waandishi Wetu
ALIYEKUWA mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi kwa tiketi ya chama cha TLP, Phares Kabuye amefariki katika ajali ya basi iliyotokea katika kijiji cha Magubike kata ya Berega wilaya ya Kilosa na kujeruhi watu 54.
Ajali hiyo ilitokea jana saa moja asubuhi katika kijiji hicho ikilihusisha basi la kampuni ya RS Investment lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam ambapo inadaiwa mbunge huyo alikuwa akiwahi mkutano mkuu wa chama cha TLP unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akitangaza taarifa za kifo hicho, jana jioni wakati wa sehemu ya pili ya kikao hicho na Mwenyekiti wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa maiti alihifadhiwa katika Hospitali ya Misheni ya Berega.
Mwenyekiti huyo, ambaye alikuwa anaendesha kikao cha bunge jana jioni, alisema kuwa taratibu za mazishi zinafanywa na familia ya marehemu.
Alisema kuwa ofisi ya bunge itawatangazia wabunge juu ya ratiba ya mazishi mara tu baada ya familia kuwapatia utaratibu.
Taarifa hiyo ilipokewa kwa masikitiko makubwa na wabunge hao hasa wakimkumbuka kwa ucheshi na umahiri wake katika kujenga hoja enzi za uhai wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio ambazo pia zimethibitishwa na kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, ajali hiyo ilitokea baada ya uzembe wa dereva wa basi hilo ambaye jina lake halijapatikana kudaiwa kumuachia kondakta wake kuendesha basi hilo.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa kondakta wa basi hilo ambaye pia jina lake halikupatikana alishindwa kulimudu basi hilo kutokana na mwendo kasi hivyo kusababisha basi hilo kupoteza mwelekeo na kupinduka ambapo watu wawili walikufa papo hapo.
Taarifa zilizopatikana zimesema Kabuye alifikwa na mauti baada ya kufikishwa katika hospitali ya Berega alikopelekwa kwa matibabu na kwamba miili ya marehemu wote watatu imehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutambuliwa na majeruhi wote wa ajali wamelazwa katika hospitali hiyo.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo inadaiwa dereva na kondakta wake walikimbia huku jeshi la polisi likiendelea na juhudi za kuwatafuta.
Phares Kabuye alizaliwa mwaka 1938 na alishawahi kuwa kada na mbunge wa chama cha mapinduzi mwaka 1977-1990 na baadae kuhamia katika chama cha TLP na kupata ubunge kwa tiketi ya chama hicho 2005 hadi alipovuliwa ubunge na mahakama mwaka juzi.
Imeandikwa na Samuel Msuya na Venance George wa Morogoro na Kizitto Noya, Dodoma wa Mwananchi.
Comments
RIP mzee Phares Kabuye.
RIP mzee Phares Kabuye.
RIP mzee Phares Kabuye.