Friday, April 03, 2009


SHAHIDI muhimu katika kesi ya Zombe na aliyedai kupata kumuona mshtakiwa nambari moja Abdallah Zombe akiwapiga risasi na kisha yeye mwenyewe akawapakia kwenye gari na kuwapeleka Muhimbili, Koplo Rashid Lema, amefariki dunia.

Lema ni mshitakiwa nambari 11 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva wa teksi, jijini Dar amefariki dunia alfajiri ya leo katika hospitali ya Ocean Road jijini, alikohamishiwa baada ya kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa muda.

Marehemu Koplo Lema ni mmoja wa washtakiwa tisa katika kesi hiyo, akiwemo mshtakiwa namba moja, Abdallah Zombe, ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wa Dar es Salaam na ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam.

Koplo Lema, ambaye ni shahidi muhimu wa utetezi kulingana na maelezo yake ya awali katika kesi hiyo, alilazimika kulazwa Muhimbili akitokea katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke alikokuwa amelazwa tangu kiasi cha wiki tatu zilizopita, baada ya uvumi kuenea wkamba ameshavuta.

Taarifa kutoka kwenye vyanzo vya gazeti la Mwananchi ndani ya taasisi hiyo zilisema kwamba juzi usiku mshitakiwa huyo alinyanyuka mwenyewe kitandani na kuanza kutembea wodini huku akiimba kwa lugha isiyoeleweka ambayo inasadikika kuwa ni ya Kiarabu,huku akisoma dua kwa kuchanganya lugha.

Mbali na kitendo hicho cha kuimba na kusoma dua pia Koplo Lema anadaiwa kuwafokea askari wa Jeshi la Magereza wanaomuangalia gherezani hapo walipojaribu kwenda kumzuia,akiwataka wamuache huku akiwatuhumu kuwa ndio wanaomuua.

Habari hizo zinasema kuwa baada ya kuamuka kitandani Koplo Lema alianza kutembea mwenyewe kuelekea kwenye mlango wa kutoka nje ya wodi hilo, huku akiimba kwa sauti inayosikika vizuri jambo ambalo linaashiria kuwa ameanza kupata ahueni.

“Tulishangaa kumuona Lema akitembea mwenyewe huku akiongea vizuri kabisa.Alikuwa akiimba kwa lugha ya ajabu ajabu hivi huku akioomba dua kwa kuchanganya na Kiswahili kuwa Mungu nisaidie, Allah Akbar,” vilisema vyanzo vyetu mbalimbali kutoka ndani ya taasisi hiyo.

No comments: