IDADI kubwa ya wanachama waliokuwa katika taasisi kupanda na kuvuna pesa ya Development Entrepreneurships Community Initiative (Deci) wamejiunga na taasisi nyingine ijulinakayo ya Tumaini.
Taasisi hiyo ambayo makazi yake makuu ni Jijini Dar es Salaam inajishughulisha na shughuli kama za Deci ingawa kuna tofauti ndogo zilizojitokeza pindi wanachama hao wanapotaka kujiunga kwa sababu wanaambiwa kuwa waingize fedha zao katika akaunti yao iliyopo katika benki ya Dar es Salaam Community Bank(DCB).
Mmoja wa wanachama wapaya kutoka Deci ya mabibo alisema kuwa, riba inayotolewa na tumaini ni kubwa ambayo wanaamini kuwa inaweza kuwapunguzia makali ya maisha pindi wanapoitwa kuvuna.
“Tumeamua kujiunga na Tumaini, tumeambiwa kuwa wanatoa riba kubwa hasa unapoingiza fedha kuanzia kiasi cha Sh100,000 hadi 200,000 na kupata Sh500,000 faida ambazo ni nyingi na unaweza kupunguza baadhi ya majukumu ya kimaisha,”alisema mwanachama huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Aliongeza mpaka sasa zaidi ya wanachama 30 ambayo walikuwa wote katika taasisi ya Deci wameamua kujiunga na Tumaini ili waweze kufidia pesa zao zilizopo Deci ambazo mpaka sasa hawana uhakika kama watalipwa au la, jambo ambalo linawafanya watafute mbinu nyingine za kupata fedha.
Alisema baadhi ya wanachama waliowekeza Deci wengi wao walikuwa wamekopa, wakati serikali imetangaza kuzifunga akaunti za Deci wamechanganyikiwa kwa kuhofia madeni ambayo walitegemea kurudisha wakati wa mavuno, jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira magumu. Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta wa Mwananchi.
Comments