Deci ni noma- Pinda



WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema shughuli za Kampuni ya DECI (Development Enterprenueurship Community Initiative) za wanachama kuweka fedha kupata faida marudufu ni sawa na upatu na ni kinyume cha sheria za nchi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo alisema ndiyo maana Serikali imeunda timu ya kuingalia DECI na kuchukua hatua bila kuwaathiri wanachama wa DECI.

“Hakuna cha maono wala ufunuo, DECI ni upatu tu. DECI siyo mkombozi ni ujanja ujanja ambao ambao lazima utaleta matatizo hatimaye,” alisema.

Shughuli za upatu ni kinyume cha sheria Na. 8 ya mwaka 2006, iliyoidhinishwa na Rais Januari 5, mwaka 2007, kuwa ni kosa kuendesha shughuli za upatu ambao hauna usalama wa fedha watu wazochanga, aliongeza.

Alisema kuwa timu iliyoundwa na serikali kuangalia shughuli za DECI ina wataalamu kutoka Benki Kuu, Wakala wa Soko la Mitaji na Dhamana (Capital Markets Authority) na Idara ya Polisi.

DECI ilianza shughuli zake nchini mwaka 2007 na iliandikishwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA).

Comments