Sunday, April 19, 2009

Si Yanga wala Simba


Kelele za wababe wa soka nchini Tanzania jana zilifikia ukingoni baada ya kila mmoja kutoka na lake. Kiufupi hakukuwa na mbabe walianza Simba wakapachika bao wakatamba wakaruka ruka na kuzomea, soka likatandazwa watu wakabaki midomo wazi, ikawa sasa wanavizia mtu akosee wazomee.

Jerry Tegete alizima kelele na shangwe za mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za ziada na kufanya matokeo kuwa 2-2 kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mashabiki wa Simba walikuwa wakishangilia kipindi chote cha mchezo na furaha yao ilizidi baada ya winga wake Ramadhani Chombo 'Redondo' kuunganisha kwa kichwa krosi ya Henry Joseph dakika ya 23 kuandika bao la kwanza kwa wekundu hao.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari kwa Simba na kufanya mashambulizi na hadi mapumziko walikuwa wakioongoza kwa bao 1-0.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Ben Mwalala aliisawazishia Yanga dakika ya 48 na kukimbilia eneo walipo mashabiki wa Simba na kuwafunga mdomo kitendo kilichowakera na kuanza kurusha chupa za maji.
Hata hivyo dakika ya 62, mchezaji bora wa mechi hiyo Haruna Moshi 'Boban' aliifungia timu yake bao la pili baada ya kuuwahi mpira ulipanguliwa na kipa Juma Kaseja baada ya kulitema shuti la Ramadhani Chombo.

Moshi alionyesha mchango mkubwa kwa timu yake jambo lilopelekea jopo la ufundi kumtangaza mchezaji bora wa mechi na kuzawadiwa shilingi 300,000 .
Bao hilo la Boban lilidumu hadi dakika 90 kabla ya Jerry Tegete kuzima furaha za mashabiki wa Simba baada ya kuunganisha krosi ya Mike Barasa kwa kifua na kumwacha kipa wa Simba, Ally Mustapha asijue la kufanya.

No comments: