Maelfu ya wanachama wa Taasisi ya Development Entrepreneurship Community Initative (Deci) kutoka sehemu mbalimbali nchini, jana walifurika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, kujua hatima yao kutoka kwa uongozi wa taasisi ulioitisha mkutano huo.
Katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa PTA katika viwanja hivyo, huku mvua kubwa ikinyesha, viongozi hao walimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa makini na ushauri wa kuifungia taasisi hiyo kwa kuwa umetolewa na wachache katika misingi ya unafiki.
Viongozi hao ambao walidai kutoyumbishwa, walitangaza kuendelea na shughuli zao na kuitaka serikali kutokurupuka kuchukua maamuzi.
Umati huo wa watu uliokadiriwa kukaribia ule wa watu wanaofika katika viwanja hivyo kwa ajili ya maonyesho ya SabaSaba kila mwaka, ulihudhuriwa na wanachama kutoka mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Lindi.
Kadiri muda ulivyosonga, idadi ya wanachama ilizidi kuongezeka na wengi wao walifika kwa magari binafsi na usafiri wa daladala.
Comments