Dar es Salaam, Julai 04, 2025 — Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, leo ametembelea banda la Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) lililopo katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ridhiwani alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Bodi hiyo ikiwa ni pamoja na usajili na utoaji wa ithibati kwa waandishi wa habari nchini, elimu kuhusu maadili ya uandishi wa habari, pamoja na mikakati ya kuboresha taaluma hiyo kwa manufaa ya umma.
Akipokea maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa JAB, Mhe. Waziri alielezwa kuwa Bodi hiyo imeendelea kupokea maombi ya ithibati kutoka kwa waandishi mbalimbali wa habari kote nchini, huku ikisisitiza umuhimu wa uandishi wa habari wenye weledi, uadilifu na uwajibikaji.
Mhe. Ridhiwani Kikwete alipongeza kazi kubwa inayofanywa na JAB katika kuhakikisha uandishi wa habari nchini unaendeshwa kitaaluma, huku akihimiza waandishi wa habari – hususan vijana – kujitokeza kwa wingi kupata ithibati ili kutambulika rasmi na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.
"Naipongeza JAB kwa kazi nzuri. Nawasihi waandishi wa habari, hasa vijana, kuchangamkia fursa ya kupata ithibati. Hii inaleta heshima kwa taaluma yenu, lakini pia ni hatua muhimu ya kujenga uwajibikaji na weledi katika kazi zenu za kila siku," alisema Mhe. Ridhiwani.
Aidha, Mhe. Waziri alitumia fursa hiyo kuzungumza na baadhi ya waandishi waliokuwepo katika banda hilo, ambapo alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa waandishi wa habari na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya habari na taasisi za serikali.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo alimshukuru Mhe. Ridhiwani kwa kutembelea banda lao na kuonesha kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Bodi katika kusimamia taaluma ya habari. Alisema ujio wa Waziri ni kichocheo kikubwa kwa Bodi kuendelea na jitihada zake za kuimarisha weledi na maadili ya uandishi nchini.
Matukio mbalimbali yaliambatana na maonesho ya vitabu vya mwongozo wa Ithibati, nyaraka za kisheria, pamoja na video fupi zinazoonesha kazi za JAB na miongozo ya utoaji ithibati kwa waandishi wa habari.