Monday, August 23, 2010

Pengo: Wanasiasa wengine wapumbavu



BAADHI ya waanasiasa nchini wameelezwa kuwa wana tabia za kipumbavu ambazo hazina tofauti na zile za wanasiasa nchini Ruanda ambao kwa upumbavu wao waliweza kusababisha maafa ya mauaji ya halaiki mwaka 1994.

Askofu mkuu Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar-es-Salaam Mwadhama Policarp Kadinali Pengo alilazimika kutumia kauli hiyo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma kutokana na kile alichokisema kuna baadhi ya wanasiasa ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwazuia viongozi wa dini kuhubiri habari njema.

Kadinali Pengo ambaye alikuwa akizungumza na halaiki katika kilele cha maadhimisho ya mwaka wa mapadri nchini alisema kuwa kitendo cha baadhi ya viongozi wa dini kuhusihwa katika matukio maovu mfano Mapadri ambao kwa kushirikiana na wanasisa dhalimu waliweza kujihusisha katika mauaji ya halaiki, si sahihi maana si viongozi wote wa dini wenye tabia chafu kama hiyo.

Alisema kauli mbaya dhidi ya viongozi wa dini zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa zimekuwa zikitolewa makusudi kwa malengo ya kuwafanya wananchi wasiwe na imani na viongozi wao wa dini vivyo hivyo kuwafanya viongozi wa dini wakate tamaa na kuacha kuhubiri kuhusu habari njema hasa kukemea maovu yanaweza kujitokeza miongoni mwa jamiii ambayo kwa namna moja au nyingine yangeweza kusababisha maafa kwa taifa.

Alisema endapo viongozi wa dini watayasikia maneno na kauli za baadhi ya wanasiasa aliyewaita wapumbavu watakuwa hawana tena thamani katika jamii endapo watashindwa kuwapuuza wanasiasa hao na kuendelea na changamoto ya kuleta tumaini jipya kwa jumuiya ya maskini.

“Nyinyi (mapadri) msidanyanyike, kwa sababu hata hao mapadri walioshiriki katika mauaji ya halaiki nchini Ruanda walivutwa na wanasiasa wapumbavu ambao walifikiri wanaweza kutwaaa nchi kirahisi kwa mbinu ile chafu,......”,

“Hatuwezi kukataa kuwa kuna mapadri sasa wapo magerezani wamehukumiwa kwa kujihusisha na mauaji hayo ya halaiki, hili lisitukatishe tamaa sisi tukihitajika kufanya utume kwa kuhubiri habari njema, waache wanasiasa waende zao maana wanasiasa wapumbavu sio wapo tu nchini Rwanda, tunao hata hapa Tanzania, kusema mapadri wasisikilizwe ni kukosa akili,”alisema Pengo. Picha na Habari za Israel Mgussi, Dodoma.

No comments: