Mrema: Vunjo wamenileta mtetea



MWENYEKITI wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema jana alitembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 kwa miguu kuudhihirishia umma kuwa yuko fiti alipokwenda kuchukua fomu za kugombea Ubunge Jimbo la Vunjo, huku akifurahia wanaCCM kumletea mgombea ambaye yeye alimwita mtetea na yeye (Mrema) ni jogoo atakayempanda mtetea huyo.

Mrema akifuatana na mgombea Urais wa TLP,Mutamwega Mganywa walitembea kwa miguu kutokea kijiji cha Chekereni kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi mji mdogo wa Himo huku akisindikizwa na mamia ya wanachama wa TLP.

Wanachama hao wakiwa wamevalia fulana za njano zenye nembo ya TLP na maneno "Vunjo hatudanganyiki" walikuwa wakishangilia huku vijana waliokuwa wakiendesha pikipiki zaidi ya 40 wakifanya vituko mbalimbali kama ishara ya kushangilia.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kukabidhiwa fomu hizo,Mrema aliwapongeza wanachama wa CCM wa Jimbo la Vunjo kwa kuamuangusha Mbunge aliyemaliza muda wake, Aloyce Kimaro katika kura za maoni.

“Wana-CCM Vunjo ni watu wazuri sana hongereni sana kwa sababu kitu kikubwa mlichokifanya ni kumuondoa Kimaro kwa sababu anapesa nyingi na angenisumbua sana lakini mmeniletea Mtetea na mimi ni Jogoo”alitamba Mrema.

Katika mchakato wa kura za maoni,wakili na mwanasheria wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Chrispin Meela aliongoza kwa kupata kura 7,732 dhidi ya Kimaro aliyepata kura 3,207 na hivyo kushindwa kutetea kiti chake.

Huku akitumia misemo ya Kiswahili kufikisha ujumbe wake wakati akiwaomba wananchi wa Jimbo hilo wasimsaliti, Mrema aliwaambia wananchi hao siku zote hajawahi kuwaomba samaki wakampa Nyoka na anaamini hawatamsaliti.

Mrema alisema ameamua kugombea Ubunge Jimbo la Vunjo kwa kuwa anasukumwa na dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi ikiwamo kuongeza uzalishaji wa kahawa bora na kutatua kero ya maji mji wa Himo.

Lakini Mgombea aliwaomba wananchi hao wamuwezeshe kuwa Mbunge kwani ana siri nzito ya namna alivyokamata vigogo wakiwa wanatorosha dhahabu nje ya nchi na mahali pekee anataka kutoboa siri hiyo ni Bungeni.

Mrema alisema aipokamata dhahabu hiyo yenye thamani ya sh175 Milioni kwa wakati huo, alimwita Inspekta Jenerali na kumuuliza wawachukulie hatua gani watuhumiwa hao lakini mkuu huyo wa polisi akashikwa na kigugumizi.

“Nikamwendea Rais wangu Mpendwa Mwinyi (Ali Hassan) nikamwambia Mheshimiwa Rais tuwafanyeje hawa watuhumiwa naye nikaona anashikwa na kigugumizi na hivi sasa wanatanua huko Kariakoo,”alidai Mrema.

Comments

Anonymous said…
JAMANI HUYU MZEE HANA WATOTO AU WAJUKUU WAJE WAGOMBEE MAANA KAZEEKA BADO ANAPENDA MADARAKA SASA INA MAANA HAJIONI AU HANA WASAHAURI MAANA KAZEEKA LKN BADO KING'ANG'ANIZI TU ATAKUJA KUFIA JUKWAANI JAMANI HIZI NI NJAA AU MAANA NA UHAKIKA HANA JIPYA WATU WA VUNJO KUENI MAKINI ACHANENI NA VIONGOZI WASIOKUA NA MSIMAMO KWANI HANA CHA KUJIVUNIA KTK JIMBO HILO ZAIDI KIMARO BORA HATA MBATIA ANGERUDI AMEFANYA MENGI BIG UP MBATIA MREMA HUNA ISHU WEWE NI KIGEUGEU PUMZIKA ACHIA VIJANA
Anonymous said…
KWELI MFA MAJI HAISHI KUTAPATAPA.MIMI NAISI HUYU MZEE KAPOTEZA CHANEL, MARA ACHEZE NGOMA NA CCM, HANA LA KUTUELEZA HUYU ZAIDI YA KUTUVURUGA KAA CHONJO HUNA JIPYA