SHIRIKA la Ndege la Precision linalotoa huduma bora Tanzania, limetangaza kuleta ndege yake mpya ya sita aina ya ATR42-500 itakayowasili Agosti 26 mwaka huu kutoka Toulouse, Ufaransa, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza programu ya kutoa huduma za kisasa zaidi. Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Precision Air, Alfonse Kioko, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa, ndege hiyo mpya itakayopachikwa jina la Bukoba, itafuatiwa na nyingine ya saba itakayoingia Septemba 15 mwaka huu.
Mwaka 2006, Precision na ATR ya Ufaransa walisaini mkataba wa dola za Marekani milioni 129 ili kutoa ndege saba mpya. Ndege ya kwanza kati ya hizo iliwasili Machi 2008. Tangu wakati huo, Precision imepokea ndege tano aina ya ATR 72-500 na kufanya iwe na ndege tano mpya mpaka sasa. Pia ina ndege nyingine tatu za zamani. Kioko alisema baada ya ndege hiyo yenye namba 5H-PWF kuwasili, wataizindua Dar es Salaam Agosti 27.
Alisema ina vifaa vya kisasa vya burudani kwa ajili ya wasafiri kuangalia sinema na kusikiliza muziki wakiwa safarini. Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 70. Mkurugenzi huyo pia alitangaza kwamba tangu kuanza mwaka mpya wa fedha, idadi ya abiria wapya imeongezeka kwa asilimia 12 kulinganisha na mwaka jana. Pia mizigo ya biashara imeongezeka licha ya kudorora kwa uchumi duniani.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja Masoko wa Precision, Emillian Rwejuna alisema kampuni hiyo inatarajia kupata ndege ya Boeing 737, kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu. Rwejuna alisema kupatikana kwa ndege hiyo kutapanua wigo wa huduma za safari.
Ndege hiyo ya tatu aina ya Boeing 737 itaboresha safari za Johannesburg, Afrika Kusini, na pia katika miji ya Kinshasa na Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Precision Air hivi sasa inafanya safari katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Musoma, Shinyanga, Kigoma, Kilimanjaro, Zanzibar, Mtwara na Arusha. Pia ina safari za Nairobi na Mombasa, Kenya na Entebbe, Uganda. Taarifa ya Precision Air
Comments