Sunday, August 22, 2010

JK aanguka jukwaaani


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwa vikwazo baada ya mgombea wake wa urais, Jakaya Kikwete kuanguka jukwaani.

Tukio hilo lilitokea jana mchana wakati mgombea huyo anayetetea nafasi yake ya urais akizindua kampeni hizo za CCM katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Saalam.

Rais Kikwete aliwasili katika viwanja hivyo saa 7:45 mchana akifuatana na Mgombea Mwenza, Dk Mohamed Gharib Bilal na kupanda katika jukwaa kuu kuungana na viongozi kadhaa wa CCM na serikali akiwa na furaha.
Rais Kikwete alianza kuhutubia saa 9:07 alasiri akitaja mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, dakika 16 baada ya kuanza kuhutubia umati wa wanaCCM waliofurika katika viwanja hivyo alinza kuishiwa nguvu na kasha kupepesuka, lakini walinzi wake walimdaka na kumpa msaada kwa kumdoa jukwaani.

Rais aliondolewa jukwaani na kupelekwa kwenye gari maalum la wagonjwa lililokuwepo uwanjani hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.

Baada ya dakika 14 baadaye alirejea jukwaani akiwa uso wake ukiwa unaonyesha kuchoka ambako aliendelea na hotuba yake kwa dakika tano kabla ya kwenda kuketi meza kuu kwa dakika mbili na kasha kuondoka katika viwanja hivyo.

Akiwa amesindikizwa na walinzi zaidi ya watano kurudi jukwaani, Kikwete alisema,"CCM oyee. Jamani nimefungulia ila niliishia kwenye suala la rushwa.''

Kitendo hicho cha rais Kikwete kukata ghafla hotuba yake kwa mara ya pili kiliwashtua mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo na kusababisha baadhi yao kuanza kulia.

Umati wa watu hao wakiwa wengi wamevaa nguyo za rangi ya kijani na njano ambayo ni rangi ya CCM ulingubikwa na vilio na kelele huku kila mmoja akizungumza maneno yake.

Tukio hilo lilishuhudiwa na familia yake akiwamo mkewe mama Salma, baadhi ya watoto wake, mama Salma Kikwete na marais wastaafu na viongozi wa serikali na chama.

Mama Salma Kikwete alishtuka baada ya tukio hilo, huku baadhi ya watoto wake wakilia.

Baadhi ya viongozi waliokuwepo hao ni marais wastaafu Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume.

Wengine ni mke wa Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere, Maria Nyerere, Mke wa Marehemu Karusme, Mama Shadya Karume, Edward Lowassa, Salim Ahmed Salim, Ali Mohamed Shein na Shamsi Vuai Nahodha.

Mara baada ya Kiwete kuondoka kwenye viwanja hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati alitangaza kuwa hotuba aliyoitoa mgombea huyo, imefungua rasmi kampeni za chama hicho.

''Jamani Rais Kikwete ndio ameshafungua rasmi kampeni za CCM, kwa hiyo huko mikoani na hapa Dar es Salaam watu waanze kampeni. Rais Kikwete amepata tatizo kidogo ila limekwisha, lakini burudani bado zipo. Mnaopenda burudani endeleeni kuwepo katika viwanja hivi, wapo Ze Comedy hapa,'' alisema Chiligati.

Kuanguka kwa mgombea huyo kuligeuza shangwe zilizotawala uwanjani hapo tangu asubuhi kutawaliwa na vilio.

Gazeti hili lilishuhudia zaidi ya watu 15 waliovalia sare za CCM wakianguka chini na kupoteza fahamu huku mmoja wao ambaye alikuwa amevaa kanzu, akinusurika kupigwa kwa kile walichomhisi wenzake kuwa ni mchawi.

Mtu huyo ambaye alikuwa amevaa nguo nyeusi na kilemba cheupe, alianza kuzongwa na wananchi alipoanza kunyanyuka alipokuwa amekaa kiwanjani hapo baada ya kumwona Rais Kikwete akidondoka.

Hata hivyo, aliokolewa na askari polisi waliokuwa karibu na eneo hilo na kumpeleka katika Kituo Kidogo cha Polisi Jangwani kilichopo mita 100 kutoka katika eneo hilo.

Baadhi ya watu waliopoteza fahamu kutokana na mshtuko wa tukio hilo walipelekwa katika vituo vya msalaba mwekundu vilivyokuwa vikitoa huduma ya kwanza uwanjani hapo.

''Jamani siwezi kujizuia inauma sana,'' alisikika mwanachama mmoja akisema kabla kuanguka na kupotesa fahamu.

Tukio hilo lilionekana kama limewatia uchungu wanachama wa CCM kwani baada ya rais Kikwete kuondoka hakuna mwanachama aliyetaka kubaki katika viwanja hivyo licha ya burudani ya vikundi na wasanii mbalimbali iliyokuwepo.

Kikwete alifika uwanjani hapo akitokea ofisi ndogo za CCM-Lumumba akisindikizwa na msafara wa pikipiki zaidi ya 200, magari na watembea kwa miguu waliokuwa wakiimba nyimbo za kumsifu mgombea wao.

Hili ni tukio la nne kwa Rais Kikwete kupatwa na mkasa wa aina hiyo, wakati akiwa jukwaani akihutubia.

Tukio la kwanza lilitokea kwenye viwanja hivyo hivyo vya Jangwani Oktoba 30, 2005, wakati anahitimisha kampaeni za chama hicho. Siku hiyo Kikwete akiwa mgombea wa CCM alionekana aliishiwa nguvu ghafla na kudondoka, kasha kundolewa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Baadaye ilitolewa taarifa kwamba, uchunguzwa na daktari umenyekana kuwa ni mzima na kwamba hali hiyo ilisababishwa na uchovu ulitokana na pilika nyingi za kampeni na wakati huo huo alikuwa anafunga kwa kuwa ulikuwa ni mwezi Mtukufu wa Waislamu.
Tukio la pili, ilikuwa Oktoba 4, mwaka jana wakati akihutubia mamia ya watu katika maadhimisho ya miaka 100 ya Kanisa la African Inland (AIC) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo, vilieleza kwamba Rais Jakaya Kikwete aliishiwa nguvu jukwaani kisha kubebwa wasaidizi wake kumpeleka katika chumba maalumu kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza. Taarifa zaidi soma www.mwananchi.co.tz

No comments: