Sunday, May 03, 2009

Rostam amvaa Mengi



MFANYABIASHARA maarufu nchini Rostam Aziz ameamua kuweka kando haya na heshima aliyokuwa nayo kwa mfanya biashara mwenzake ambaye wakati fulani alidai kwamba ni mzee kuliko baba yake na akamsema kuwa ndiye 'Fisadi Nyangumi'.

Rostam Aziz, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara watano waliotuhumiwa na Mengi kuwa mapapa wa ufisadi, jana alitoa mlolongo wa tuhuma za ufisadi dhidi ya mwenyekiti huyo mtendaji wa makampuni ya IPP, na kueleza bayana kuwa atawasilisha vielelezo kwa vyombo husika ndani ya saa 48 ili Mengi aanze kuchunguzwa.

Mapigo ya Rostam, ambayo yanazidi kupandisha joto la vita hiyo ya maneno, yametokana na tuhuma nzito ambazo Mengi alizitoa Aprili 23 wakati alipotaja wafanyabiashara watano akitaka wadhibitiwe mapema, akiwemo mbunge huyo wa Igunga.

Tofauti na Mengi ambaye hakutoa vielelezo na kusema yuko tayari kupandishwa kizimbani ili ukweli udhihirike, Rostam aliorodhesha tuhuma nyingi na kuahidi kuzikabidhi kwenye vyombo vya serikali ili hatua zichukuliwe.

Rostam alianza kwa kuorodha matukio 10 ya ugomvi ambayo anadai Mengi aliuanzisha dhidi ya watu mbalimbali- kuanzia maaskofu hadi kikundi cha uchekeshaji- wakati kwa mujibu wa Rostam maslahi ya Mengi ya kibiashara yalipoingiliwa na baadaye kuyageuza kuwa ni ugomvi wa nchi nzima.

"Sasa ameanzisha ugomvi na mimi baada ya kuona kwamba mimi nimekuwa mshindani wake mkubwa katika umiliki wa vyombo vya habari hapa nchini, anataka kuufanya ugomvi wa nchi nzima," anaeleza Rostam.

Akiorodhesha tuhuma za ufisadi dhidi ya Mengi, Rostam alidai mwenyekiti huyo wa IPP alianza kuifilisi nchi kwa kushiriki kwenye vitendo vilivyochangia kuifilisi Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kusababishwa iuzwe "kwa bei poa".

1 comment:

Anonymous said...

Duu.Mshikaji ila nikunong'oneze kidogo..kuacha utani mzee una meki kinoma yaani unatucha watupu kweli mshikaji ila tufanyeje nawe uko jikoni basi ILA USIMWAMBIE MTU