WANAFUNZI kutoka shule za serikali wameweza kuongoza katika watahiniwa kumi bora kwa jumla kitaifa akiwemo msichana mmoja tu katika kundi hilo na wote walioshika nafasi hizo walikuwa wakisoma masomo ya mchepuo wa sayansi (PCM).
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta Dk. Joyce Ndalichako wanafunzi hao kumi bora kwa jumla kitaifa wanatoka shule za sekondari za Kibaha, Tabora Boys, Ilboru na Mzumbe.
Watahiniwa hao kumi kwa jumla kitaifa aliyeshika namba moja ni Auden Kileo (Kibaha Sekondari), Raymond Aidan(Kibaha Sekondari), Frank Shega (Tabora Boys), Charles Simkonda(Ilboru Sekondari), Maclean Mwaijonga (Feza Boy's), Sophia Nahoza(Marian Girls), Atupele Kilindu (Mzumbe Sekondari), Athuman Juma (Ilboru Sekondari), Dickson Mutegeki (Tabora Boy's) na Michael Andrew(Ilboru Sekondari).
Matokeo hayo yameonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa shule kimeongezeka kwa asilimia 1.65 huku kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea kikishuka kwa asilimia 6.56 ikilinganishwa na mwaka jana.
Kwa watahiniwa wa shule waliofaulu ni 36,472 sawa na asilimia 94.37 ya watahiniwa wa shule waliofanya mtihani na idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 9,244 sawa na silimia 74.84 ya watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani mwaka huu.
Wasichana waliofaulu ni 17,152 sawa na asilimia 90.92 ya wasichana waliofanya mtihani, wakati wavulana waliofaulu ni 28,564 sawa na asilimia 88.89 ya wavulana waliofanya mtihani.
Alisema kwa kuangalia ubora wa ufaulu kwa madaraja waliyopata watahiniwa wa shule katika mtihani huo unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 32,023 sawa na asilimia 82.86 wamefaulu katika madaraja I hadi III na wasichana waliofaulu katika madaraja I hadi III ni 12,053 sawa na asilimia 82.84 na wavulana ni 19,970 sawa na asilimia 82.87. Imeandikwa na Boniface Meena
Comments