Kesi ya Mahalu yahama



KESI ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh 2 bilioni inayomkabili aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na mwenzake imehamia mahakama kuu baada ya washtakiwa hao kuomba kupitiwa upya kwa mwenendo wa kesi yao.

Mahalu na aliyekuwa ofisa utawala wa ubalozi wa Tanzania nchini Italia Grace Martin jana walitakiwa waanze kujitetea baada ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaona kuwa wana kesi ya kujibu.

Hata hivyo kabla ya Mahalu hajaanza kujitetea mmoja wa mawakili wa upande wa utetezi Cathbert Tenga alisimama na kuwasilisha hoja kadhaa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Sivangilwa Mwangesi anayesikiliza kesi hiyo.

Tenga alidai kuwa upande wa utetezi umewasilisha maombi katika Mahakama Kuu ukiomba kupitiwa upya kwa mwenendo wa kesi hiyo.

Akijibu hoja hiyo Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Ponsiano Lukosi alidai kuwa kutokana na maombi hayo ya upande wa utetezi Mahakama ya Kisutu inatakiwa isimamishe usikilizwaji wa kesi hiyo ili kuwezesha jalada la kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu.

“Mheshimiwa hakimu naomba mahakama itoe mwongozo juu ya suala hili kwasababu hatuwezi kuendelea na kesi hadi jalada la kesi hii litakaporudi kutoka Mahakama Kuu,”alisema Lukosi.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Mwangesi alitoa uamuzi kuwa mahakama ya Kisutu haitaendelea kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa maombi ya washitakiwa.

Akizungumza nje ya mahakama, wakili Tenga alisema kuwa wameamua kupeleka maombi hayo mahakama kuu kwasababu kesi hiyo si ya rushwa lakini wanashangaa kuona inaendeshwa na maafisa wa Takukuru. habari na Nora Damian

Comments