Friday, May 29, 2009

Liyumba sasa mambo yake supa


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa masharti mapya ya dhamana kwa Mkurugenzi zamani wa Utawala na Utumishi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh 221 bilioni.

Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba alisema mahakamani hapo jana kuwa amekubaliana na hoja za upande wa utetezi kwamba kifungu namba 148 hakiingiliani na kesi hiyo.

“Hakuna ubishi kwamba mshitakiwa ana haki ya kupata dhamana kwa sababu kifungu walichokitaja upande wa mashitaka hakiingiliani na kesi hii,” alisema Hakimu Nyigulila.

Katika masharti hayo, Liyumba anatakiwa kutoa Sh 300 milioni au hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha pesa, kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh 50 milioni kila mmoja, kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na kuwasilisha polisi hati yake ya kusafiria.

Awali Liyumba alipewa dhamana katika mazingira ya utatanishi baada ya hati zake nyingi kuonekana zina kasoro, lakini akaruhusiwa kurudi uraiani kwa hati ya mali ya Sh882 milioni kati ya Sh55 bilioni zinazotakiwa kwa dhamana.

Upande wa utetezi ulisema mahakamani hapo kuwa uko tayari kwa ajili ya dhamana, lakini upande wa mashitaka ulidai kutokuwa na muda, hivyo Hakimu Mwaseba akaahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi mwaka huu itakapoendelea kwa ajili ya dhamana.

Upande wa mashitaka juzi uliiomba mahakama kutumia kifungu namba 148 (5) (e) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ambacho kinaeleza wazi kwamba mshitakiwa anaweza kutoa nusu ya pesa zilizoibwa au hati ya mali.

Hata hivyo upande wa utetezi kupitia kwa wakili Majura Magafu ulidai kuwa kifungo kilichotajwa na upande wa mashitaka hakistahili kutumiwa katika kesi hiyo kwa madai kwamba mashitaka ya mteja wake ni ya matumizi mabaya ya ofisi ambayo katika kifungu hicho hayapo.

No comments: