Aliyekuwa Mkurugenzi wa utumishi wa BoT, Amatus Liyumba na Meneja mradi wa benki hiyo Deogratias Kweka wameachiwa huru na Mahakama ya Kisutu leo baada ya kubaini kuwa hati ya mashitaka ina makosa ya kisheria.
Uamuzi huo ulitolewa leo na Hakimu Mkazi Wariyalwande Lema anayesikiliza kesi hiyo. Baada ya kutolewa uamuzi huo saa 5:20 asubuhi washitakiwa hao walishuka kizimbani na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Washitakiwa hao walipelekwa katika moja ya vyumba vilivyoko mahakamani hapo na saa 5:34 asubuhi walichukuliwa na Defender la polisi lenye namba T 337AKV.
Wakati wa kesi hiyo ulinzi uliimarishwa mahakamani hapo kwani kulikuwa na askari polisi zaidi ya watano waliokuwa wamevaa kiraia huku wakiwa wameshikilia bunduki.
Mmoja wa mawakili wanaowatetea washitakiwa hao Hudson Ndusyepo alisema wateja wao wamepelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Pia mawakili hao wanataka shitaka la tatu linalowakabili wateja wao la kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh 221 bilioni liondolewe kwani halijawekwa wazi kwamba washitakiwa wamefanya kosa gani.
Katika hoja za upande wa Jamuhuri kupitia kwa wakili wa serikali Boniface Stanslaus ulikiri mahakamani kukosewa kwa hati hiyo lakini uliiomba mahakama iwaruhusu ili waweze kuwabadilisha hati mpya.
Comments