Friday, October 24, 2008

Vigogo wa harakati za albino


Mwenyekiti wa Good Hope Star Foundation,Al-Shaymaa Kwegyir, akitoa taarifa ya asasi hiyo kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete

Mwanaharakati na mfanyabiashara mwenye ulemavu wa ngozi (albino) kutoka Canada, Peter Ash, ameiomba serikali kuingiza katika mitaala ya shule za msingi na sekondari elimu kuhusu albino ili kusaidia kupunguza mauaji yanayoendelea nchini.

Akizungumza katika mkutano wake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi, Dar es Salaam jana, Ash aliyewasili nchini juzi na ujumbe wa watu watatu, alisema kinachoisumbua jamii ni uelewa mdogo kuhusu albino ni watu gani.

Alisema wameridhika na juhudi za Serikali ya Tanzania katika mapambano, zinazoongozwa na Rais Jakaya Kikwete na hatua zilizotangazwa kuwa zitachukuliwa kwa watakaobainika, lakini bado elimu kuanzia ngazi za shule za misingi inahitajika kwa manufaa ya kizazi kijacho.

“Kinachoonekana kwa mataifa mengi ni elimu duni kuhusu sisi tunatokeaje, wengi hawaelewi kwamba tu binadamu wa kawaida, tofauti yetu ni ngozi inayotokana na ukosefu wa vinasaba vya aina fulani katika miili yetu, hili linahitajika kufundishwa kwa mapana zaidi,” alisisitiza Ash.

Ash, ambaye anatarajia kwenda Mwanza kukutana na familia zilizoathirika kwa mauaji hayo, alisema binafsi kama mwanaharakati wa kupinga mauaji hayo ya kinyama, ataendelea kushirikiana kwa karibu na serikali, lakini pia pamoja na asasi za kijamii zinazoonyesha wazi kupambana na mauaji hayo.

Aliiomba serikali kutoa ulinzi imara kwa familia zenye albino na jamii kushiriki kuwafichua wauaji ili hatua zilizotajwa na Rais Kikwete zichukuliwe. Kwa mujibu wa Ash, ambaye pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa asasi ya kijamii ya Under the Same Sun inayohusika na haki za watu wenye ulemavu hususani albino nchini Canada, duniani wapo albino zaidi ya 5,000 na wengi wao wapo katika nchi za Kiafrika, Tanzania ikiwamo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Balozi Iddi alimhakikishia Ash kuwa serikali itahakikisha usalama kwa albino na itachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuhusika katika mauaji hayo.

No comments: