TANZANIA YATEULIWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 37 WA SHIRIKA LA MAKAZI AFRIKA 2018

● Kunufaika na kuvutia  watalii
● Ni mkutano unaovuta wawekezaji na wafanyabiashara
● Mkutano huo huhuzisha nchi wanachama 44 wa Afrika

Na Muungano Saguya, Victoria Falls, Zimbabwe
Tanzania imeteuliwa kwa kauli moja na wajumbe wa Mkutano wa 36 wa Makazi Afrika(Shelter Afrique) kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 37 ambao utafanyika mwezi Julai 2018 Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ambao una wanachama kutoka nchi 44 za Afrika walikutana katika Mji wa Kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe ili kujadili changamoto za hali ya makazi kwa watu wa nchi hizo ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo kwa kutumia uzoefu wa kila nchi mwanachama. Aidha, katika Mkutano huo ambapo Tanzania iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Kyando Mchechu, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi, iliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo wa 36.
Mambo mbalimbali yalijadiliwa na kukubalika ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto ya Rasilimali Fedha  inayozikabili nchi nyingi wanachama wa Umoja huo na kushindwa kuwapatia wananchi wa Afrika makazi bora na nafuu. Katika kuondoa changamoto hiyo Mkutano huo umeazimia kuongeza Daraja C la wanachama wa umoja huo ambalo litahusisha mashirika, taasisi za kifedha  na nchi za nje ya bara la Afrika ili kupata fedha au kuwa na ubia wa pamoja wa kusaidia kuwapatia wananchi wan chi wanachama makazi bora na nafuu. Kadhalika, nchi hizo za kiafrika zimekubaliana kuhakikisha kila nchi inakamilisha michango yake inayodaiwa ili kuwezesha umoja huo kuendelea kusaidia mikopo kwa nchi wanachama ya kugharamia miradi ya ujenzi wa nyumba. Kundi A la Umoja huo huhusisha nchi 44 za Afrika na Kundi B huhusisha Benki ya Afrika(ADB).
Kuteuliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 37 kumechangiwa na Wajumbe wengi kufurahishwa na mabadiliko yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na Rais Dkt John Pombe Magufuli amekuwa gumzo kubwa kwa Wajumbe wa Mkutano huo wa Makazi kila walizungumzia changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.
Faida zitakazopatikana katika Mkutano huo kufanyika nchini Tanzania ni pamoja na kukuza utalii wa Tanzania kwa Wajumbe hao kuelezwa fursa za utalii na kujionea kazi mbalimbali za wajasiriamali hususan wa sekta ya nyumba ambao hualikwa katika Mkutano huo. Aidha, ni fursa kubwa kwa nchi kujitangaza kibiashara na kuvutia wawekezaji kutoka Bara la Afrika.
Tanzania ilijiunga na Shelter Afrique mwaka 2003 na Mkutano wa 32 wa Shelter - Afrique uliofanyika N’djamena, Chad mwaka 2013 ulipitisha Azimio Namba GM/2013/005 la kuongeza Hisa kwa kila nchi mwanachama kwa lengo la kukuza mtaji wa kampuni hiyo na kuiwezesha kuweka nguvu zaidi katika masuala ya uendelezaji nyumba barani Afrika.
Shirika la Nyumba la Taifa limenufaika na mtaji huo ambapo mwaka 2002 lilikopeshwa Dola za Kimarekani 1.5 milioni na kuzitumia kujenga nyumba 212 eneo la Boko Jijini Dar es Salaam na mwaka 2011 lilikopeshwa fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 14.5 milioni mkopo uliotakiwa kurejeshwa katika kipindi cha miaka 10 na mkopo huo ulitumika kujenga nyumba za gharama nafuu zipatazo 558 katika maeneo mbalimbali nchini. Pamoja na kuikopesha NHC, Shelter Afrique imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani 27,500,000/= katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba nchini Tanzania.
Mkutano huo wa 36 umefanyika katika Mji wa Kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe zamani ikiitwa Southern Rhodesia, ambapo wajumbe walipata pia fursa ya kutembezwa kwenye vivutio vya kitalii vilivyopo katika Mji huo unaopakana na nchi ya Zambia, zamani ikiitwa Nothern Rhodesia.





Comments