Thursday, July 27, 2017

DSG yaandaa maonesho ya mji wa kisasa Fumba (Fumba Town Development)

Muonekano wa ramani ya Mji mpya wa Fumba unaosimamiwa na Kampuni ya DSG kutoka Ujerumani ambao utatambulishwa rasmi kwa wananchi tarehe tano na sita mwezi ujao. 
Ofisa Mkuu wa Operesheni katika Kampuni ya DSG inayojenga mji wa kisasa Fumba, Tobias Dietzold, akizungumza na waandishi wa habari kuelezea maandalizi ya kuutambulisha mradi wao. Mkutano huo umefanyika ofisini kwao Migombani mjini Zanzibar. 
Meneja Mauzo wa Kampuni ya DSG inayojenga mji wa kisasa na nyumba za makaazi katika kijiji cha Fumba, Said Ally Said, akitoa ufafanuzi wa masuali yaliyoulizwa na waandishi wa habari katika mkutano wa kuutambulisha mradi wao kwa wananchi. 

Picha na Makame Mshenga. 

………………………………………………………… 

Na Salum Vuai Maelezo Zanzibar. 

Kampuni ya DSG inayoendesha ujenzi wa mji wa kisasa katika kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi B, imeandaa maonesho maalumu ili kuutambulisha mradi huo kwa wananchi wa Zanzibar na watu mbalimbali kutoka maeneo mengine. 

Ofisa Mkuu wa Operesheni katika kampuni hiyo Tobias Dietzold, amewaambia waandishi wa habari kuwa, maonesho hayo yatakayofanyika Agosti 5 na 6 mwaka huu, yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Mkurugenzi wa ZIPA Salum Khamis Nassor na wananchi mbalimbali. 

Alisema mradi huo uliopewa jina la ‘Fumba Town Development’, unalenga kuunga mkono mipango ya serikali katika kuyabadilisha maisha ya Wazanzibari, ambao kama walivyo watu wa nchi nyengine, wanahitaji makaazi bora pamoja na huduma nyengine muhimu za kijamii. 

Dietzold aliwatoa wasiwasi wananchi wa visiwa hivi ambao hawana uwezo mkubwa wa kifedha, akiwataka wafute dhana kwamba nyumba hizo zinajengwa kwa ajili ya matajiri, akisema bei zake zinapishana kulingana na aina ya nyumba zenyewe. 

Alifahamisha kuwa kampuni yake imeandaa usafiri wa mabasi wa uhakika na wa kutosha kuweza kuwasafirisha watu watakaopenda kwenda Fumba kujionea maonesho na jinsi mji huo unavyojengwa. 

Aidha amesema maandalizi yamefanywa kwa watu watakaohudhuria kupata huduma mbalimbali zikiwemo za chakula na vinywaji. 

Naye Mkuu wa kitengo cha mauzo katika kampuni hiyo Said Ali Said, amesema mradi huo uliofunguliwa rasmi mwezi wa Agosti 2015, na kuanza ujenzi Oktoba mwaka jana, umefikia hatua nzuri ambapo takriban nyumba 75 zimeshaezekwa zikiwemo za ghorofa nne.

No comments: