JAFO AFURAHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI IHUNGO

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akifanya ukaguzi wa miundombinu inayojengwa katika Shule ya Sekondari Ihungo. 
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari Ihungo. 
Jengo la bweni linalojengwa katika shule ya Sekondari Ihungo. 
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akikagua majengo yanayojengwa katika Shule ya Sekondari Ihungo. 
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Omumwani wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo 

……………………………….. 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa shule ya wavulana ya kidato cha tano na sita ya Ihungo ambayo majengo yake yalibomoka kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka Jana. 

Kutokana na kubomoka kwa majengo hayo, Serikali iliamua kuijenga upya kwa kutumia wakala wa majengo Tanzania (TBA). Akiwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali mkoani Kagera, Jafo alitembelea shuleni hapo kukagua ujenzi wake. 

Naibu Waziri Jafo aliwapongeza wakandarasi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti. Akizungumza na wananchi waliokuwepo katika eneo hilo, Jafo alisema serikali imeamua kuijenga sekondari hiyo kisasa zaidi. Alisema sekondari hiyo inatarajiwa kuwa sekondari ya mfano ndani ya Tanzania kwa kuwa na majengo ya kisasa zaidi kuliko sekondari zote hapa nchini. 

Hata hivyo, Jafo alitoa angalizo kwa sekondari hiyo kubaki kuwa sekondari ya wavulana kwani kutokana na uzuri wa miundombinu ya kisasa inayojengwa isije baadae wakaja watu na kubadilisha mawazo kuwa Chuo kikuu jambo ambalo sio sahihi. 

Alibainisha serikali imejipanga kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kwasasa. Katika ziara hiyo, Jafo pia alitembelea shule ya Omumwani ambayo imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano ambao ni wasichana kwa mwaka huu. Alitoa maagizo kwa manispaa ya Bukoba kumalizia ukarabati wa maabara ndani ya wiki mbili zijazo ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vyema zaidi katika masomo yao kivitendo.

Comments