Tuesday, March 21, 2017

Maonyesho ya biashara ya Mauritius yazinduliwa Dar

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara chini, Johnson Minja akizungumza kwenye warsha fupi  ya uzinduzi wa maonyesho biashara ya Mauritius yaliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo yanayohusisha makampuni mbalimbali kutoka nchini Mauritius yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa baina ya nchi hizo mbili kujenga mahusiano na kutizama fursa za kibiashara baina yao
Ofisa Biashara Mkuu wa Tantrade, Stephen Kobro akizungumza kwenye warsha fupi  ya uzinduzi wa maonyesho biashara ya Mauritius yaliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo yanayohusisha makampuni mbalimbali kutoka nchini Mauritius yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa baina ya nchi hizo mbili kujenga mahusiano na kutizama fursa za kibiashara baina yao.

 Maonyesho ya biashara yanayohusisha makampuni mbalimbali kutoka nchini Mauritius yamezinduliwa leo jijini Dar es Salaam yakilenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa baina ya nchi hizo mbili kujenga mahusiano na kutizama fursa za kibiashara baina yao.

Maonyesho hayo ya siku mbili yameratibiwa na kampuni ya Talemwa Investment Consulting Company (TICC) ya nchini Tanzania, kwa kushirikiana kampuni za Enterprise Mauritius (EM) Mauritius na apex Trade Promotion Organisation Mauritius za nchini Mauritius huku yakihusisha zaidi ya makampuni yaliyojikita kwenye sekta za kilimo, uhandisi, nguo na usafi kutoka nchini Mauritius.

Akizungumza kwenye warsha fupi ya uzinduzi wa maonyesho hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo,  Mkurugenzi wa TICC, Bw. David Lutabana alisema maonyesho hayo ni fursa ya kipekee itakayowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili ili kuweza kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili fursa za kipekee zilizopo baina ya nchi hizo.

“Mauritius ni miongoni mwa nchi ambazo zinakuja juu kwa kasi kiuchumi na zinaweza  kuwavutia wawekezaji kutoka nchini Tanzania kwenda kuwekeza kule wakati huo huo tunatarajia kwamba Tanzania ikiwa kama kitovu cha biashara na maliasili mbalimbali inaweza kuwavutia pia wawekezaji kutoka Mauritius kuja kuwekeza huku,’’ alisema.

Aliongeza kuwa katika maonyesho hayo ambayo pia yatatoa fursa kwa wahusika kujifunza tamaduni tofauti na zile za mataifa yao, mada mbalimbali zitawasilishwa sambamba na mikutano kadhaa baina ya wahusika kutoka pande hizo mbili.

Akizungumzia maonyesho hayo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara chini, Johnson Minja alitoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kutafuta fursa mbalimbali za kibiashara ili kujiongeze masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Uwepo wa maonyesho haya ni wazi utaendelea kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa kitanzania kuweza kutambua fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo nje ya nchi. Lakini pia maonyesho haya yatafungua milango kwa wenzetu kutoka Mauritius kutuletea mawazo na mbinu mpya kibiashara. Nawasihi sana wafanyabiashara wa Kitanzania wachangamkie sana fursa hii,’’ alisisitiza.

No comments: