WIZARA YA HABARI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUKEMEA VITENDO VYA MMOMONYOKO WA MAADILI NCHINI.

KEME
Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura (Kulia) akizungumza na wadau wa Sekta ya Utamaduni (hawapo pichani) walioshiriki katika kikao cha Wadau tuzungumze kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Lily Beleko
KEME 1
 Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Lily Beleko akifafanua jambo wakati wa kikao na wadau wa sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam
KEME 2
Mkurugenzi wa Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Bw. Bernard James akichangia mada wakati wa kikao na wadau wa sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam
KEME 3
 Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza akijibu hoja za wadau wakati wa kikao na wadau wa sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam
KEME 4
Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura (Katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya utamaduni walioshikiki kikao cha wadau kujadili namna ya kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini leo Jijini Dar es Salaam. Kulia waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Leah Kihimbi
Picha na: Genofeva Matemu – WHUSM
……………
NA: Shamimu Nyaki – WHUSM.
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo imewataka wadau wa Sekta ya Utamaduni na jamii kwa ujumla kusaidiana katika kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili ambao umekuwa kikwazo katika kuulinda Utamaduni wa mtanzania.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa anazungumza na Wadau wa Sekta ya Utamaduni katika muendelezo wa kikao cha “WADAU TUZUNGUMZE” ambapo amesema kuwa suala la mmomonyoko wa Maadili linaanzia ngazi ya familia hivyo linapaswa kukemea kwa nguvu zote.
“Suala la mmomonyoko wa maadili ni mtambuka na huanzia ndani ya familia na huendelea kujigawa kulingana na umri, rika, na hatimaye jamii kwa ujumla hivyo ni budi watu wote kulikemea ili tuwe na jamii yenye maadili mazuri”, Alisema Mhe. Anastazia.
Aidha Mhe. Anastazia ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kutoa elimu kwa kuwatumia maafisa Utamaduni wa kila Mkoa  ili kuhakikisha suala la mmomonyoko wa maadili linashughulikiwa kwa kina kwa kuwa Wizara ndio yenye dhamana ya kuratibu na kusimamia maadili ya jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Lily Beleko amesema kuwa Idara yake inafanya juhudi kubwa za uhamasishaji wa jamii nzima kwa kushughulikia mipango madhubuti ya kuanzisha mifumo ya kudhibiti mmomonyoko wa maadili hapa nchini.
“Suala hili la maadili linahusu jamii nzima hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhusisha na kushirikisha jamii yote kuchangia katika mjadala wa kupata njia sahihi za kupambana na mmomonyoko wa maadili ya jamii yetu.”Alisema Bibi Lily.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano Baraza la Maaskofu Tanzania Bw. Bernad James ameishauri Serikali kuendelea kukemea vitendo vyote vinavyosababisha maadili kumomonyoka hasa udhibiti wa maudhui katika sehemu tofauti ikiwemo  Muziki na Filamu ambayo ndio maeneo yanayohusisha watanzania wengi.
Kikao cha “WADAU TUZUNGUMZE” kilichoanzishwa na Mhe. Waziri wa Habari Utamaduni  Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye kwa lengo la kukutana na wadau na kujadili changamoto zilizopo katika Wizara yake na namna ya kuzitatua  leo kimeshirikisha Wadau wa Sekta ya Utamaduni ambapo  mada ya leo ilikuwa “Je Maadili rasmi ya Mtanzania yapo au hayapo”.

Comments