Sunday, March 12, 2017

Sir George Kahama afariki dunia leo

ALIYEITWA na Mwalimu Nyerere kuingia katika serikali ya kwanza ya wazalendo kwenye madaraka ya ndani 1958 Sir George Kahama amefariki dunia leo saa kumi akiwa katika idara ya magonjwa ya dharura na ajali Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .
Kwa mujibu wa msemaji wa Muhimbili, John Steven Mtumishi huyo wa umma wa mstaafu na mwanasiasa wa muda mrefu mwenye uvumilivu mkubwa alifuikishwa hospitalini hapo Ijumaa.
Msemaji huyo hakuwa tayari kueleza tatizo lililomfikisha  hospitalini, lakini alisema kwamba alifikwa na umauti wakati akifanyiwa uchunguzi.
Mzee Kahama ambaye amekuwa mtumishi wa umma aliyekuwa mtendaji mkuu na mwanasiasa aliye mahiri na makini, katika utendaji kazi kuanzia nyakati za Tanganyika kudai uhuru mnamo miaka ya 1950, hadi kujitawala mwaka 1961 alikuwa rafiki wa karibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Sir George pamoja na kushika nafasi mbalimbali kati ya mwaka 1987 na 1990 alikuwa Balozi wa Tanzania nchini  China. Sir George, aliteuliwa na Nyerere mwishoni mwa utawala wake kabla ya kung’atuka mwaka 1984, aende kuwa Balozi wa Tanzania China.
Katika Serikali ya madaraka ya mwaka 1958, alikuwa Waziri wa Ushirika na Masoko na mwenyewe (Nyerere) akiwa Waziri Mkuu. 
Baadhi ya mawaziri walioteuliwa katika serikali hiyo walikuwa Paul Bomani, Chifu Abdallah Fundikira, Rashid Mfaume Kawawa, Solomon Eliofoo, Nsilo Swai, Said Maswanya, Dereck Noel Bryceson, Sir. Ernest Versey na Amir Jamal.
Serikali ya Madaraka iliendelea kuwapo sambamba na ya kikoloni na ilipofika  Desemba 9, 1961 kama ilivyoahidiwa na Umoja wa Mataifa, Tanganyika ilitangazwa kuwa huru, na Baraza la Mawaziri lenye madaraka kamili likaundwa, Sir George akiwa waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mbali ya nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali, Sir George alipata kuteuliwa kuanzisha taasisi nyeti za kimaendeleo, zikiwa ni pamoja na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Viwanda (NDC); Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA); na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

No comments: