TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE NA TAASISI YA OPEN HEART YA NCHINI AUSTRALIA YAFANYA UPASUAJI WA MOYO KWA WAGONJWA 11

JKC-2

Na Anna Nkinda – JKCI
14/3/2017 Jumla ya wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ushirikiana na madaktari wenzao wa Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji wa Moyo Bashir Nyangasa wakati akielezea jinsi kambi hiyo ya upasuaji inavyoendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa.
Dkt. Nyangasa alisema, “Kwa kushirikiana na washirika wetu wa OHI tulianza kambi maalum ya upasuaji kuanzia tarehe 10/03/2017 hadi leo  tarehe 17/3/2017 tumefanya  upasuaji kwa wagonjwa 11 ambao wanaendelea vizuri,  kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima ni wawili”,.  
Dkt. Nyangasa alisema  katika kambi hiyo  ambayo inamalizika tarehe 17/3/2017 walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 25 kati ya hao watoto ni 15 na watu wazima ni 10.
Kuhusu uhitaji  wa damu kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa Moyo Dkt. Nyangasa alisema wagonjwa hao wanahitaji damu nyingi hivyo basi aliwaomba wananchi wajitokeze kuchangia  damu ambayo itatumika kwa wagonjwa.
“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na  uchangiaji huu wa damu  usifanyike mara moja bali  uwe endelevu  kwani Taasisi inatoa huduma kwa wagonjwa wakati wote siyo wakati wa kambi maalum za matibabu ya moyo pekee yake”, alisisitiza Dkt. Nyangasa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu  wa 2017 JKCI kwa kushirikiana na baadhi ya washirika wake wa nje ya nchi ambao ni  Madaktari  Afrika wa  Marekani, Hospitali za  Apolo Bangalore na BLK zote za nchini  India na Open Heart International ya Australia wamefanya  matibabu ya moyo ya kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Comments